UMASIKINI unaochochewa na ukosefu wa mavuno kutokana na athari za
mabadiliko ya tabianchi, umeendelea kuwatikisa wakulima katika vijiji
vya Wilaya ya Chamwino, mkoani Dodoma.
Hivi karibuni, mwandishi wa makala haya alifika katika vijiji vya
Chamwino, Buigiri, Chinagali II na Mwegamile katika Tarafa ya Chilonwa
na kuzungumza na wakulima, wafugaji pamoja na wadau wengine wa kilimo.
Katika makala haya, anaeleza namna ambavyo utekelezaji madhubuti wa
mipango na mikakati ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi,
unavyoweza kupunguza kama si kukomesha umasikini unaochochewa na
uzalishaji mdogo katika kilimo.
Uzalishaji mdogo umejidhihirisha zaidi katika msimu wa mwaka 2016/17
ambao Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chamwino, Athumani Masasi anasema upo
upungufu wa tani 4,949 za chakula.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, takribani hekta 83,208 za mazao ya
chakula zililimwa na zikazalishwa tani 82,569 za chakula. Mahitaji
halisi ya wilaya hiyo yalikuwa tani 87,518. Kulingana na sensa ya watu
na makazi ya mwaka 2012, wilaya ina wastani wa watu 330,543 na wastani
wa watu 4.5 kwa kaya.
Akielezea namna uzalishaji ulivyoshuka, mkulima katika kijiji cha
Buigiri, Olivia Chinyemba anasema mwaka 2015 alilima ekari moja ya mtama
na kuvuna gunia tatu; mwaka jana akapata gunia mbili. Mwaka huu amepata
gunia moja la uwele na kwa upande wa mahindi, katika ekari moja amepata
debe moja.
Kwa upande wake, mkazi wa Kijiji cha Chinangali, Michael Mbena, mwaka
juzi alilima ekari moja ya mahindi akaambulia gunia nne na ekari moja
ya uwele alikopata gunia tano. Mwaka 2016/2017 alilima shamba la ukubwa
huo huo akapata gunia mbili na nusu na uwele akapata gunia tano.
Mwaka huu anasema hakupata chochote. Ofisa Mifugo wa Kata ya Buigiri,
Stephano Adeline, ingawa hana takwimu rasmi za uzalishaji katika
kilimo, anakiri mavuno yamekuwa yakishuka mwaka hadi mwaka kuanzia 2014.
“Takwimu kamili sina ila naongea kulingana na ninachokiona.
Mwaka 2014 mavuno yalikuwa mazuri, hata mwaka 2015 mazao yalianza
vizuri lakini ilipofika mwishoni , mvua ikakatika,” anasema Adeline
akisisitiza kuwa msimu wa 2016/17 hali imekuwa mbaya zaidi.
Asilimia tano ya wakulima 40 waliozungumza na mwandishi wa makala
haya kwa nyakati tofauti kutoka vijiji hivyo vya Chamwino, Buigiri,
Chinangali II na Mwegamile, wanaamini hakuna namna ya kukabili njaa na
umasikini endapo mvua zitaendelea kutotabirika.
“Sisi hatuna majibu, bali tunamwachia Mungu... Ofisa Kilimo
utambanaje? Kwani yeye ana chakula? Mungu ndiye anayejua hili tatizo la
ukame. Tunamwachia Mungu mipango yake,” anasema mkulima wa Chinangali
II, Michael Mbena.
Lakini pia wakulima 14 sawa na asilimia 35 ya waliohojiwa wanasema
wataalamu, hususani maofisa ugani ndiyo wanapaswa kuja na suluhisho la
uzalishaji mdogo unaochangia umasikini.
Mathalani, Japhet Mdachi, ambaye ni mkulima katika Kijiji cha
Buigiri, anasema, maofisa kilimo na mifugo wa vijiji na kata wasisubiri
mikutano ya hadhara ndipo wawape ushauri wa kuhimili ukame. Kadhalika,
wakulima 24 sawa na asilimia 60 wanasema serikali ndiyo yenye suluhisho
wakimaanisha halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Wizara ya Kilimo na
Rais.
Hata hivyo, wakulima wote walipohojiwa kama wanaelewa mipango,
miongozo au mikakati ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi katika kilimo,
walisema hawafahamu. Pia baadhi ya maofisa ugani, wanasema hawafahamu
vizuri mipango hiyo, Ofisa Mifugo wa Kata ya Chamwino, David Msimbe
anasema: “Mimi ninachokiona, mabadiliko ya tabianchi, nayaelewa kwa
sababu nimesoma.
Lakini mpango mkakati wa kitaifa au wa kiwilaya, kwetu sisi tunakuwa
hatufahamu vizuri. Hatujui wilaya imejipangaje. Tunatumia uzoefu tu wa
kule chuoni ni namna gani ya kuwasaidia wakulima.”
Mpango wa Kilimo wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi wa mwaka
2014-2019 (ACRP) ni miongoni mwa mipango ambayo wakulima, maofisa ugani,
halmashauri na wadau wengine wanapaswa waielewe na kuitekeleza.
ACRP umeainisha maeneo, mikakati na mbinu za kilimo kinachohimili
mabadiliko chenye tija kama vile udhibiti wa maji katika ardhi ikiwamo
kilimo cha umwagiliaji, uvunaji wa maji na kuyahifadhi na kilimo cha
matuta.
Mbinu nyingine zinazoainishwa katika mpango huu ni kuhusu mbegu bora
huku mpango ukisisitiza matumizi ya mbegu fupi zinazohimili ukame;
uboreshaji wa taarifa za hali ya hewa na kuhakikisha zinawafikia
wakulima.
Wapo wanaohimiza Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuandaa kalenda mpya
ya kilimo, kwani inasemekana yapo matukio ya wakulima kupishana na
kipindi cha mvua kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Programu ya Kitaifa ya Kilimo Kinachohimili Mabadiliko ya Tabianchi
ya mwaka 2015 ni mkakati mwingine wa serikali. Programu hii ni dira kwa
sekta ya kilimo, ikilenga kuhimili mabadiliko ya tabia nchi na kuwa na
usalama wa chakula kwa maendeleo ya uchumi yanayoendana na Dira ya
Maendeleo ya Taifa 2025.
Upo pia Mwongozo wa Kilimo Kinachohimili Mabadiliko ya Tabianchi
uliozinduliwa Mei mwaka huu ambao maofisa mipango na maofisa ugani
wamepewa nguvu ya kupanga na kuandaa bajeti kwa ajili ya maendeleo ya
kilimo kinachohimili mabadiliko ya tabianchi katika jamii
wanazozitumikia.
Maofisa ugani wanatakiwa kuhamasisha na kufundisha wakulima kutumia
mbinu za kilimo zinazohimili mabadiliko ya tabianchi kama vile uvunaji
na utunzaji wa maji ya mvua; umwagiliaji kwa njia ya matone; hifadhi ya
udongo na maji pamoja na kilimo cha matuta.
Mwongozo unataja Bima ya Mazao kuwa ni mbinu nyingine ya kuwaepusha
wakulima kuingia hasara na hatimaye umasikini kutokana na athari za
mabadiliko ya tabianchi. Kuhusu bima ya mazao, Mratibu wa Bima ya Mazao
katika Shirika la Bima la Taifa, Prosper Peter anasema lengo ni kumfidia
mkulima ikiwa mazao yameharibiwa na mvua au ukame yakiwa shambani.
Hata hivyo, Prosper anasema shirika lake halijaingiza rasmi bima hii
sokoni. Lakini anasema itakapoingia hivi karibuni, imejielekeza kwenye
mazao ya biashara. Aidha anasema hakujawa na utaratibu maalumu wa
kumsaidia mkulima mdogo asiye na uwezo wa kuchangia katika mfuko wa
bima.
“Baadhi ya nchi za wenzetu kumekuwa na utaratibu wa serikali
kuchangia gharama ya bima ya mazao lakini Tanzania hakujawa na utaratibu
kama huo,” anasema Prosper. Ofisa Tathimini na Ufuatiliaji wa Taasisi
ya Dodoma Network Environment (DONET), Emmanuel James katika kuelezea
suluhisho la tatizo, anasisitiza halmashaui kuweka kipaumbele kwenye
utekelezaji wa mbinu za uhifadhi wa ardhi na maji ikiwamo kuendesha
kilimo cha umwagiliaji.
James anashauri mbinu hizo ziende sambamba na kuwapa wananchi njia
nyingine za kujipatia kipato wasitegemee kilimo pekee. Anatoa mfano wa
ufugaji wa nyuki kuwa ni shughuli isiyohitaji mvua nyingi inayoweza
kufanyika wilayani Chamwino na wakulima wakajipatia kipato.
Shirika limekwishatoa mizinga 60 kwa vijiji vya Idifu (wilaya ya
Chamwino) na Kikombo (Manispaa ya Dodoma) kila kimoja. Pia kijiji cha
Mayamaya na Asanje vimepewa mizinga 38 kila kimoja lengo likiwa ni
kuwezesha jamii kujipatia kipato.
Katika kuelezea suluhisho la tatizo, Mkurugenzi wa Shirika la Climate
Action Network (CAN) linaloshughulika na masuala ya mabadiliko ya
tabianchi, Sixbert Mwanga, anahimiza wakulima kupatiwa utabiri wa hali
ya hewa ulio sahihi, unaojielekeza kwenye eneo mahususi.
Mwanga ambaye ni mtaalamu wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi,
anasema: “Siyo mkulima apewe utabiri wa jumla. Mfano utabiri unaotaja
kuwa mvua itanyesha katika Kanda ya Kati, au utabiri unaosema mvua
itanyesha mkoa wa Dodoma, hautoshi.
Mkulima asaidiwe kutumia taarifa za hali ya hewa zilizo sahihi,”
anasema Mwanga. Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga anataja
suluhisho lingine la tatizo ni wakulima kuzingatia mwongozo wa
uzalishaji mazao kulingana na kanda za kilimo za kiikolojia badala ya
kung’ang’ania mazao yasiyostawi katika maeneo yao.
Afisa Tarafa ya Chilonwa, Mohammed Mfaki anasema katika msimu ujao,
wamepanga atakayelima mahindi zaidi ya inavyoshauriwa, hawatasita
kuyafyeka kwa lengo la kuwafanya wakulima watii ushauri wa kitaalamu.
Anatoa mfano kuwa baadhi ya wakulima wameendelea kupanda mahindi ambayo
hayastawi katika maeneo yao.
Kulingana na mwongozo huo, mazao ya kipaumbele ya chakula katika
Wilaya ya Chamwino ni mtama na njugu mawe na ya biashara ni zabibu na
ufuta. Mazao mengine yanayoweza kulimwa ni alizeti, karanga mpunga na
viazi vitamu.
Mwongozo huo umezingatia ikolojia ya wilaya hii yenye mwinuko wa meta
500 -1,400, mvua milimita 400 – 800 na udongo mwekundu na kichanga.
Mkuu wa Idara ya Mazingira katika Wizara ya Kilimo, Shakwaanande Natai
anasisitiza kuwa suluhisho ni mipango, miongozo na mikakati ya kilimo
kinachohimili mabadiliko ya tabianchi kuwafikia wakulima