Mkataba baina ya Iran na mataifa makubwa sita umeanza kutekelezwa baada
ya shirika la kudhibiti matumizi ya nyuklia duniani IAEA kuthibitisha
kwamba Iran imezitimiza dhima zake juu ya mkataba huo
Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif mjini Vienna
Iran imeondolewa vikwazo na jumuiya ya kimataifa vilivyouathiri uchumi
wa nchi hiyo kwa kiwango kikubwa na kwa muda mrefu. Lakini itahitaji
kiasi cha dola nusu Trilioni ili kuurekebisha uchumi wake.
Umoja wa Ulaya na Marekani zimetangaza kuviondoa vikwazo dhidi ya Iran
baada ya kuhakikishiwa na shirika la IAEA kwamba nchi hiyo imevitekeleza
vipengele vyote vya mkataba wa kihistoria,juu ya mpango wake wa nyuklia
iliotiliana saini na mataifa makubwa sita, pamoja na Umoja wa Ulaya,
mnamo mwezi wa Julai mwaka uliopita.
Marekani imefahamisha kwamba Iran sasa itaweza kuzipata fedha zake,
kiasi cha dola Bilioni 50 zinazotokana na mali zake zilizokuwa
zinashikiliwa katika nchi za nje. Kwa mujibu wa taarifa, mali za Iran
zilizokuwa zinashikiliwa katika nchi za nje zinafikia thamani ya dola
Bilioni 100.
Hata hivyo nchi hiyo inahitaji kiasi cha dola nusu Trilioni ili
kuurekebisha uchumi wake uliothiriwa kwa muda mrefu na vikwazo vya nchi
za magharibi.
Busara, mdahalo na ushirikiano zaleta tija
Waziri Javad Zarif akizungumza na waandishi habari mjini Vienna
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammed Javad Zarif na Mkuu wa
sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini walithibitisha
kuondolewa kwa vikwazo walipozungumza na waandishi wa habari katika mji
mkuu wa Austria,Vienna.
Moghrerini amesema, kutokana na Iran kuitekeleza sehemu yake ya mkataba,
vikwazo vya kimataifa, vya kiuchumi na vya kifedha vilivyowekwa na
jumuiya ya kimataifa dhidi ya Iran vimeondolewa. Mkuu wa sera za nje wa
Umoja wa Ulaya amesema makubaliano yaliyofikiwa na Iran ni imara na ya
haki.
Muda mfupi baada ya mkutano na waandishi habari, Waziri wa mambo ya nje
wa Marekani John Kerry naye alithibitisha kwamba Marekani pia imeviondoa
vikwazo ilivyoweka dhidi ya Iran. Rais Barack Obama pia alitia saini
agizo la kuzibatilisha hati juu ya kuiwekea Iran vikwazo.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema tarehe 16 ni
siku nzuri kwa Iran,Mashariki ya Kati na kwa dunia nzima. Waziri Javad
Zarif ameeleza kuwa kufanya mdahalo, kuheshimiana, na diplomasia ndiyo
mambo yaliyoleta suluhisho, na siyo vitisho, vikwazo na mashinikizo.
Shirika la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia limesema wakaguzi
wake walioenda nchini Iran waliweza kuthibitisha kwamba nchi hiyo
imezitimiza dhima zake zote juu ya mkataba iliyoutia saini na mataifa
makubwa sita pamoja na Umoja wa Ulaya.
Rais Iran Hassan Rouhani alitumia mtandao wa Twitter kusifu hatua ya kuiondolea nchi yake vikwazo.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philip Hammond amesema hatua hiyo ya
kihistoria italeta usalama zaidi duniani. Waziri Hammond ameeleza
kwamba hatua ya kuanza kuyatekeleza makubaliano yaliyofikiwa na Iran ,
ambapo nchi yake Uingereza, pia ilitoa mchango mkubwa, itaifanya sehemu
ya Mashariki ya Kati na dunia yote kwa jumla kuwa salama zaidi.
Ujerumani yapongeza kuondolewa vikwazo
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema
makubaliano na Iran ni mafanikio ya kihistoria kwa diplomasia.
Hata hivyo Seneta wa chama cha Demokratik nchini Marekani Richard
Blumenthal ametaka Iran iwekewe vikwazo na Marekani kwa sababu ya
kufanya majaribio ya makombora ya masafa marefu yanayokiuka maazimio ya
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo katika kile kinachozingatiwa kuwa ni kuanza kujengeka
uhusiano mzuri baina ya Iran na Marekani nchi hizo zimebadilishana
wafungwa.
SHUDATE