Sunday, January 17, 2016

Iran yarejea katika jumuiya ya kimataifa baada ya kutengwa kwa muda mrefu

Mkataba baina ya Iran na mataifa makubwa sita umeanza kutekelezwa baada ya shirika la kudhibiti matumizi ya nyuklia duniani IAEA kuthibitisha kwamba Iran imezitimiza dhima zake juu ya mkataba huo
Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif mjini Vienna Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif mjini Vienna
Iran imeondolewa vikwazo na jumuiya ya kimataifa vilivyouathiri uchumi wa nchi hiyo kwa kiwango kikubwa na kwa muda mrefu. Lakini itahitaji kiasi cha dola nusu Trilioni ili kuurekebisha uchumi wake.
Umoja wa Ulaya na Marekani zimetangaza kuviondoa vikwazo dhidi ya Iran baada ya kuhakikishiwa na shirika la IAEA kwamba nchi hiyo imevitekeleza vipengele vyote vya mkataba wa kihistoria,juu ya mpango wake wa nyuklia iliotiliana saini na mataifa makubwa sita, pamoja na Umoja wa Ulaya, mnamo mwezi wa Julai mwaka uliopita.
Marekani imefahamisha kwamba Iran sasa itaweza kuzipata fedha zake, kiasi cha dola Bilioni 50 zinazotokana na mali zake zilizokuwa zinashikiliwa katika nchi za nje. Kwa mujibu wa taarifa, mali za Iran zilizokuwa zinashikiliwa katika nchi za nje zinafikia thamani ya dola Bilioni 100.
Hata hivyo nchi hiyo inahitaji kiasi cha dola nusu Trilioni ili kuurekebisha uchumi wake uliothiriwa kwa muda mrefu na vikwazo vya nchi za magharibi.
Busara, mdahalo na ushirikiano zaleta tija
Waziri Javad Zarif akizungumza na waandishi habari mjini Vienna Waziri Javad Zarif akizungumza na waandishi habari mjini Vienna
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammed Javad Zarif na Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini walithibitisha kuondolewa kwa vikwazo walipozungumza na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Austria,Vienna.
Moghrerini amesema, kutokana na Iran kuitekeleza sehemu yake ya mkataba, vikwazo vya kimataifa, vya kiuchumi na vya kifedha vilivyowekwa na jumuiya ya kimataifa dhidi ya Iran vimeondolewa. Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya amesema makubaliano yaliyofikiwa na Iran ni imara na ya haki.
Muda mfupi baada ya mkutano na waandishi habari, Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry naye alithibitisha kwamba Marekani pia imeviondoa vikwazo ilivyoweka dhidi ya Iran. Rais Barack Obama pia alitia saini agizo la kuzibatilisha hati juu ya kuiwekea Iran vikwazo.
Waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammad Javad Zarif amesema tarehe 16 ni siku nzuri kwa Iran,Mashariki ya Kati na kwa dunia nzima. Waziri Javad Zarif ameeleza kuwa kufanya mdahalo, kuheshimiana, na diplomasia ndiyo mambo yaliyoleta suluhisho, na siyo vitisho, vikwazo na mashinikizo.
Shirika la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia limesema wakaguzi wake walioenda nchini Iran waliweza kuthibitisha kwamba nchi hiyo imezitimiza dhima zake zote juu ya mkataba iliyoutia saini na mataifa makubwa sita pamoja na Umoja wa Ulaya.
Rais Iran Hassan Rouhani alitumia mtandao wa Twitter kusifu hatua ya kuiondolea nchi yake vikwazo.
Waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Philip Hammond amesema hatua hiyo ya kihistoria italeta usalama zaidi duniani. Waziri Hammond ameeleza kwamba hatua ya kuanza kuyatekeleza makubaliano yaliyofikiwa na Iran , ambapo nchi yake Uingereza, pia ilitoa mchango mkubwa, itaifanya sehemu ya Mashariki ya Kati na dunia yote kwa jumla kuwa salama zaidi.
Ujerumani yapongeza kuondolewa vikwazo
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier amesema makubaliano na Iran ni mafanikio ya kihistoria kwa diplomasia.
Hata hivyo Seneta wa chama cha Demokratik nchini Marekani Richard Blumenthal ametaka Iran iwekewe vikwazo na Marekani kwa sababu ya kufanya majaribio ya makombora ya masafa marefu yanayokiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo katika kile kinachozingatiwa kuwa ni kuanza kujengeka uhusiano mzuri baina ya Iran na Marekani nchi hizo zimebadilishana wafungwa.

SHUDATE

0 comments:

Post a Comment