KILIMO ni sekta inayotegemewa kiuchumi na Watanzania zaidi ya
asilimia 75, kwa mujibu wa matokeo ya utafiti wa kitakwimu uliofanywa na
mashirika tofauti ya ndani na kimataifa, Shirika la Chakula na Kilimo
la Umoja wa Mataifa (FAO), kwa mujibu wa ripoti yake ya 2013, kilimo
kinachangia asilimia 30 ya pato la ndani (GDP) na asilimia 64 ya pato
linalotokana na mauzo nje ya nchi.
Kilimo ni sekta inatoa ajira mara 11 zaidi ya sekta nyingine za
uzalishaji nchini, hivyo kuifanya kuwa na umuhimu wa pekee katika kukuza
uchumi wa nchi na kustawisha maendeleo ya watu.
Ni kutokana na umuhimu huo, mwaka jana Baraza la Kilimo nchini (ACT)
liliratibu utafiti uliojielekeza katika mifumo ya usimamizi kwa matumizi
ya pembejeo za kilimo, mnyororo wa usambazaji na namna zinavyochochea
uzalishaji kwa mkulima.
Utafiti huo uliofanywa na kampuni ya Match Maker Associates kwa niaba
ya ACT, ulielekezwa katika mikoa yenye kanda zinazonufaika na mradi wa
SAGCOT na Kaskazini mwa nchi.
Ofisa anayeshughulikia sera katika ACT, Laetitia William anasema
utafiti huo ulifanyika kwenye wilaya tatu na kuzilenga pembejeo chache
ambazo ni mbolea, mbegu na kemikali zinazotumika kwenye kilimo.
Wilaya hizo na mazao yaliyotumika katika utafiti huo kwenye mabano ni
Mbozi na Babati (mahindi), Kilombero (mpunga), Babati (alizeti na
maharage). Kwa mujibu wa ripoti ya Wizara ya Kilimo, mahitaji ya mbegu
zilizoboreshwa nchini yanakadiriwa kuwa zaidi ya tani za ujazo 120,000
kwa mwaka wakati kiasi kinachosambazwa ni tani za ujazo 35,352 sawa na
asilimia 59.
Hata hivyo, ripoti hiyo inaeleza kuwa matumizi ya mbegu hizo yapo kwa
kiwango kidogo, ikikadiriwa kwamba asilimia 25 ya mazao yanayovunwa
yanatokana na mbegu zilizoboreshwa wakati asilimia 75 ni kutoka kwenye
mbegu za asili.
Hali hiyo inatokana na ukubwa wa bei inayotozwa kwa mbegu
zilizoboreshwa, upatikanaji wake, miundombinu na mtandao duni katika
usambazaji. Mtafiti John Alinanuswe kutoka Match Maker Associate
Limited, anasema utafiti huo, pamoja na mambo mengine ulibaini kuwa
kutokana na upatikanaji fedha usiokuwa wa uhakika kwa Taasisi ya
Uthibitisho Rasmi Mbegu (TOSCI), wakati mwingine unasababisha kuchelewa
kwa utekelezaji wa majukumu inayojipangia hususani kwenye ofisi zake
zilizopo Arusha, Mwanza, Mtwara, Njombe na Morogoro.
Hali hiyo, kwa mujibu wa taarifa ya utafiti, imechangia pia sehemu ya
ziara za ukaguzi wa TOSCI kukasimiwa kwa maofisa wa serikali ngazi ya
wilaya. Alinanuswe anasema licha ya Kamati ya Taifa ya Mbegu (NSC)
kuitisha mkutano wa wadau wa mbegu mara moja kwa mwaka, lengo likiwa ni
kujadili masuala yanayohusiana na sekta hiyo, mahudhurio si ya
kuridhisha kutokana na ushiriki kuwa suala la hiari.
Hata hivyo, ripoti hiyo inakosoa kwamba vikao hivyo vinaitishwa na
kufanyika kitaifa wakati katika ngazi ya wilaya ufanisi wake ni mdogo na
mara nyingi havifanyiki kutokana na sababu tofauti ikiwamo taasisi za
wadau wa pembejeo za kilimo kutohudhuria.
Aidha, taarifa ya kitengo cha zana za kilimo katika Wizara ya Kilimo,
inaonesha kuwa mahitaji ya mbolea yaliongezeka kutoka mita za ujazo
485,000 kwa msimu wa 2011/2011 kufikia 885,019 mwaka 2015/2016.
Mtafiti Alinanuswe anasema utafiti uliofanywa umebaini kuwa
ubadilishanaji taarifa kati ya mamlaka zinazosimamia sekta ya kilimo
nchini dhidi ya wadau wanaoshirikiana nao ni mdogo. “Katika majadiliano
na mamlaka tofauti za usimamizi wa kilimo, hatukupata ushahidi wa
kumbukumbu za pamoja za wadau wanaojihusisha na uingizaji na biashara ya
pembejeo za kilimo,” anasema.
Hata hivyo, mwakilishi wa Tosci, Mtafiti Mwandamizi Doroth Ole
Meiludi anasema hali hiyo imeboreshwa na kwamba miongoni mwa mamlaka
hizo na hususani taasisi hiyo ya uthibitisho wa mbegu ina kumbukumbu
hizo zinazosaidia kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Lakini Alinanuswe anasema ukosefu wa kumbukumbu unasababisha ugumu
katika kuisimamia sekta ya kilimo, kuwatambua wanaoshiriki vitendo viovu
dhidi ya pembejeo na kuwachukulia hatua zinazostahili.
Anasema matokeo hayo yanaonesha kuwa mamlaka za usimamizi
zinakabiliwa na upungufu wa rasilimali watu na fedha, akizitaja kuwa ni
nyenzo muhimu zinazochochea ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wakati.
Kuhusu mnyororo wa usambazaji pembejeo nchini, matokeo ya utafiti huo
yanaonesha kuwapo kiwango duni cha uratibu wa pamoja wa shughuli za
taasisi zinazoundwa na kampuni za uingizaji na biashara ya pembejeo.
Kampuni hizo zipo huru kujiunga na taasisi tofauti zilizoundwa ambazo
ni pamoja na Chama cha Wafanyabiashara ya Mbegu (Tasta) na Chama cha
Mawakala wa Mbegu (Tanada).
Alinanuswe anasema taasisi hizo zimebainika kupitia utafiti huo
hazina uratibu wa pamoja na hakuna mfumo wa kuwezesha zikidhi sera na
kanuni za mfumo wa usambazaji pembejeo nchini na kwamba hazijajiunda
kusaidia shughuli za wasambazaji pembejeo kuwa na ufanisi.
Mtafiti huyo anasema stadi za utawala wa biashara kwa washiriki wengi
wa pembejeo za kilimo hazipo kwa kiwango cha kuibua uwazi na ufanisi
katika mfumo wa utoaji huduma husika.
Alinanuswe anasema ongezeko la matumizi sahihi ya pembejeo linaweza
kuchangia kuongezeka uzalishaji na faida kwa wakulima. Utafiti unabaini
kuwa sekta hiyo bado inakabiliwa na changamoto kadhaa zikiwamo ufinyu wa
masoko, ubovu wa miundombinu, ukosefu wa taarifa sahihi, fedha na bima,
hali inayoweza kufifisha ufanisi kwa wakulima, ikiwa hazitapatiwa
ufumbuzi.
Wakati huo huo utafiti umebaini kiwango cha uwapo wa pembejeo bandia
za kilimo kushuka kwa mwaka jana ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka
2012. Anasema watoa taarifa katika utafiti huo walieleza kuwa mbolea,
mbegu na viuatilifu haziwaathiri kwa kiwango kinacholingana kama
ilivyokuwa awali, akitoa mfano kada chache kama za watumishi katika
halmashauri za wilaya na wakulima pekee, walizungumza uwapo wa mbolea
bandia.
Akasema kada hizo pamoja wafanyakazi wa kampuni za mbegu walieleza
kuwa takribani asilimia 20 ya mbegu zilizopo kwenye soko zina ubora
hafifu unaoziweka katika kundi la pembejeo bandia.
Waliohojiwa katika utafiti huo, wamekaririwa wakieleza kuwa hali ya
pembejeo bandia ni mbaya zaidi kwa upande wa viuatilifu. MAPENDEKEZO
Utafiti huo unapendekeza, pamoja na mambo mengine, kuwapo mapitio yenye
lengo la kuboresha mamlaka za usimamizi katika sekta ya kilimo,
kuboresha uratibu miongoni mwa mamlaka hizo ili zifanye kazi zikilenga
kuboresha huduma kwa mkulima na kumpunguzia gharama za uzalishaji.
Mapendekezo mengine ni kutangaza kwenye gazeti la serikali majina ya
wakaguzi wa mbegu, mbolea na viuatilifu katika ngazi za wilaya na
kuwajengea uwezo ili watimize wajibu wao kwa ufanisi.
Pia kufanikisha upatikanaji wa taarifa zinazohitajika katika
kusajili, biashara na kuingiza pembejeo za kilimo. Kuongeza kiasi cha
faini kwa wahusika wa pembejeo bandia na fidia kwa waathirika wa vitendo
hivyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Janeth
Bitegeko anasema mkutano wa kujadili matokeo ya utafiti huo ni jukwaa
muhimu hasa katika kipindi hiki ambacho kasi ya utendaji kazi wa
serikali ni kubwa, hivyo kuwapo uwezekano wa upungufu kadhaa kufanyiwa
kazi tangu kufanyika kwa utafiti huo.
Bitegeko anasema kilimo ni biashara inayochangia maendeleo ya nchi,
ustawi na uboreshaji huduma za jamii kutokana na fedha zinazopatikana
kupitia kodi mbalimbali zinazotozwa kwenye sekta hiyo.
Ni kutokana na hali hiyo, Bitegeko anasema baraza limejikita katika
kujenga uwezo wa wakulima na wadau wengine wa kilimo kuhusiana na
mnyororo wa thamani ya mazao hususani katika kulima, kuvuna, kuuza na
masoko