Wednesday, October 25, 2017

UMASKINI UNAVYOPELEKEA UHARIBIFU WA MAZINGIRA


Image result for upikaji kwa kutumia jiko la kuniImage result for upikaji kwa kutumia jiko la kuni
 

NJE ya nyumba ya Emmy Lenjima, katika kijiji cha Buigiri wilayani Chamwino nashuhudia kichanja kilichosheheni kuni. Bibi huyu, Emmy (70), anaendelea kupanga hizo kuni.
Ni muda wa mchana ambao katika maeneo ya vijijini, hukosi kushuhudia moshi unaoashiria kupika kwa ajili ya maakuli, lakini nyumbani kwa bibi huyu, hakuna dalili za kupikwa chochote. Mmoja wa wanakaya, Thomas Madimilo, anaweka wazi: “Kila nyumba ina njaa... Ukibahatika kupata chakula sasa hivi (saa 6:00 mchana), utegemee tena kula kesho yake.”
Madimilo anasema siku hiyo hawakuwa na mpango wa kupika chakula licha ya kwamba, kila mmoja ametoka kuhemea chakula. Anasema hata hizo kuni anazopanga Emmy, siyo tu kwa matumizi ya kupikia nyumbani, bali huzitembeza kijijini ili apate fedha za kununulia chakula. Kaya hiyo ni sehemu ya kaya katika vjijiji vya Chamwino, Chinangali II, Buigiri na Mwegamile, wilayani Chamwino ambavyo ukosefu wa mavuno shambani, umewachochea kujihusisha na uvunaji misitu kwa ajili ya kupata kuni na mkaa ambao huuza ili kupata fedha za kununulia chakula.
Upungufu wa mvua unaochangiwa na ufyekaji misitu, umesababisha mazao kukauka na hivyo kusababisha umasikini kuongezeka. Kwa kawaida, mazao yakivunwa, hutumika kwa chakula na ziada huuzwa ili kupata fedha kwa ajili ya mahitaji mengine.
Lakini sasa, hali ni tofauti. Wakazi hawa ambao wanakiri kupata mlo mmoja kwa kuhangaika kufanya vibarua, katika kutafuta fedha za kununulia chakula, wanasema ukataji kuni umeshika kasi. Licha ya kwamba ukataji misitu unachangia ukame na hatimaye ukosefu wa chakula, lakini kuni na mkaa ndiyo ‘mradi’ ulio ndani ya uwezo wa wengi kama inavyoelezwa na Emmy. “Tunasaidiana kutafuta hela za kununua chakula.
Wanaume wanakata kuni kuchoma mkaa na kufanya vibarua, sisi tunachanja kuni zitusaidie kupata hela.” Wakati debe moja la mahindi linauzwa kati ya Sh 10,000 na Sh14,000, akina mama hawa huuza mzigo wa kuni kati ya Sh 500 na Sh 1,000 kulingana na ukubwa wa mzigo.
“Nikiuza zikaisha, narudi tena porini kuchanja,” anasema Rahel Lenjima, bibi mwingine anayekadiriwa kuwa umri wa miaka 80, mkazi wa kijiji cha Buigiri. Anasema siku zote alikuwa akikata kuni kwa matumizi ya nyumbani lakini baada ya kukosa chakula, imebidi aungane na wengine kukata kuni za biashara.
Wengi wa wakazi hawa hawafahamu juu ya athari za ongezeko la ukataji miti kwa ajili ya mkaa na kuni katika kilimo na hatimaye ustawi wa maisha yao. Cyprian Matangula anafafanua kuwa ukataji kuni kwa ajili ya matumizi ya nishati ya kupikia ni jambo la kawaida kwa wanakijiji.
“Lakini sasa kuna ongezeko la watu wanaokata kuni na mkaa kwa ajili ya kuuza ili kujiingizia kipato,” anasema Matangula na kusema sababu ni hali ya upatikanaji chakula kuwa mbaya. Matangula anakiri kufahamu athari za ukataji kuni na uchomaji mkaa kuwa ni shughuli zinazoharibu mazingira hivyo kuchangia ukosefu wa mvua.
Mwongozo wa mashirika ya MJUMITA, MVIWATA, TFCG, Action Aid na TOAM kwa wakufunzi wa mafunzo ya kilimo hifadhi ya mazingira ngazi ya vijiji, unaelezea pia kwamba uchomaji mkaa huharibu tabaka la ozoni na kuongeza kwa kiwango cha joto duniani.
Mashirika haya chini ya Mradi wa Mabadiliko ya Tabia nchi, Kilimo na kupunguza umasikini (CCAP), yanaelimisha katika mwongozo wake kuwa, kwa kawaida miti hufyonza hewa ukaa. Kwa maana hiyo, miti ikikatwa hovyo, hewa ukaa haitafyonzwa tena, badala yake itaenda kuharibu tabaka la ozoni lililoko angani ambalo kazi yake ni kupunguza ukali wa miale ya jua.
Baada ya uharibifu huo kiwango cha joto duniani huongezeka kwa kiasi kikubwa na hivyo kusababisha madhara mengi kama vile ukame na ukosefu wa mvua. Matangula anawakilisha wanakijiji wanaofahamu madhara ya ufyekaji miti, lakini ukosefu wa chakula na fedha unawalazimisha kufanya hivyo na hata yeye hana la kusaidia jamii yake.
Lucy Masigati mwenye umri wa miaka 56 anaeleza namna ambavyo hutembea takribani saa moja kutafuta kuni. Emi Chiloya, mkazi wa Buigiri anasisitiza: “Mapori yako mbali. Tunakwenda hadi huko vijiji vya mbali ili tupate kuni kubwa kubwa.”
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwegamile chenye kaya 404, Jeremiah Mpandula anasema misitu ya karibu na kijijini kwao imetoweka siyo tu kwa ukataji kuni, bali pia kutokana na kilimo na ujenzi wa nyumba. Mpandula anasema: “Miaka ya zamani, watu walichanja kuni karibu sana.
Tena kuni zenyewe za kutumia nyumbani. Sasa hivi hata hizo za kuuza wanazipata kwa shida kwenye vichaka vichache vilivyosalia.” Hata hivyo, mkazi wa Kijiji cha Chamwino, Richard Julius anasema biashara hiyo ya kuni ni ya kuganga njaa tu.
“Wala huwezi kusema watu wanapata hela nyingi za kuwafanya wapate mahitaji yote,” anasema Julius akishauri halmashauri isaidie kutatua tatizo la umasikini unaotokana na ukosefu wa mvua ili ufyekaji misitu usiendelee kushika kasi kwa lengo la kuganga njaa.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili wa Wilaya ya Chamwino, Rugambwa Banyikila, kiwango cha ufyekaji misitu ni asilimia mbili. Biashara ya mkaa ndiyo inachangia zaidi ufyekaji misitu kuliko ukataji kuni.
Kwa mujibu wa mkuu huyu wa idara, Wilaya ya Chamwino ina eneo la misitu ya asili yenye ukubwa kilometa za mraba 1960.96 na misitu ya hifadhi ni kilometa za mraa 63.08.
Idara hupata ruzuku ya sh 400,000 kwa mwezi kutoka serikali kuu ambazo hutumika kuanzisha vitalu vya miche, kupanda miche, kuitunza pamoja na kusaidia katika doria za mara kwa mara kwa ajili ya udhibiti.
Hata hivyo, Ofisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka Shirika la Dodoma Network Environment (DONET), Emmanuel James, anasema udhibiti wa uharibifu wa misitu unapaswa uangaliwe kwa jicho la kukomesha umasikini unaowakabili wanavijiji. “Mabadiliko ya tabianchi tunayaangalia zaidi kwa maisha ya watu na wanyama. Maisha ya watu yamekuwa duni. Umasikini umeongezeka.
Wanapokosa chakula, tunaangalia rasilimali nyingine kama vile misitu. Watu wasipopata mvua ya kutosha, misitu inaangaliwa zaidi kwa ajili ya kukata mkaa na kuni,” anasema James. Ukataji kuni na uchomaji mkaa katika vijiji hivi vya Chamwino, ni uharibifu wa mazingira ambao DONET inasema unahitaji mipango thabiti ya kuukabili kwa kuwapa wakulima mbinu za kupata fedha bila kuharibu misitu.
“Unaweza kuhifadhi mazingira na bado ukapata fedha. Usipohifadhi mazingira, utapata fedha kwa haraka na zitapotea mara moja,” Katibu Mkuu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais, Dk Faustine Kamuzora anasema.
Ukataji miti na uchomaji mkaa unachangia umaskini kwa sababu kadri misitu inavyotoweka, ndivyo vyanzo vya maji vinavyokauka na ndivyo mvua zinavyozidi kuwa haba. Ofisa Mifugo Mwandamizi wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Theresia Massoy anashauri wakulima kupanda miti kando ya mashamba yao yenye matumizi mtambuka, ikiwamo miti ili kuzalisha hewa ya nitrojeni.
Upandaji miti siyo kwa lengo la kupata kuni na mkaa kudhibiti ufyekaji wa misitu, bali pia kuhifadhi rutuba ya udongo na kuhifadhi maji katika mashamba. Ripoti ya Hali ya Mazingira nchini ya mwaka 2014 inaweka bayana kuwa uharibifu wa ardhi umechangia mavuno hafifu ya kilimo na kutokuwepo kwa uhakika wa chakula ambako ni kinyume na Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDGs) yaliyopitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 2015.
Malengo haya endelevu ni kutokomeza umasikini kwa kuongeza kipato cha watu. Lengo namba mbili linajielekeza kwenye kutokomeza njaa, kuwa na uhakika wa chakula,lishe bora na kukuza kilimo endelevu

0 comments:

Post a Comment