Sunday, October 22, 2017

Serikali kuvunja nyumba zilizojengwa bila kibali




Serikali imewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji kuweka alama za X na kuvunja majengo yote yanayojengwa katika miji yao bila kibali na yale yanayojengwa katika viwanja vya watu wengine walio na hati

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi ameyasema hayo alipofanya ziara wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa alpoenda kutatua mgogoro wa ardhi ambapo ameagiza eneo ya lililokuwa shamba la mifugo la Malonje wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa lenye ukubwa wa ekari 12,750, lirejeshwe serikalini kwa vile utaratibu wa kuligawa umekiukwa kwa kiwango kikubwa, na masharti ya uendeshaji hayajazingatiwa kabisa.

Waziri Lukuvi amesema tatizo la ujenzi holela lianaanza pale ambapo Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji wanaacha majengo yanaibuka katika miji yao bila kujua ujenzi huo una kibali au unajengwa katika kiwanja chenye hati na muhusika wa hati hiyo ndio anayejenga.

“Hatuwezi kuendelea na zoezi la kufanya urasimishaji wa makazi kila siku wakati chanzo cha tatizo hilo kinajulikana, kwa hiyo naagiza Wakurugenzi, Maafisa Ardhi, Maafisa Ujenzi na Maafisa Mipangomiji kuweka x katika majengo yote yanayojengwa bila vibali na ujenzi unaofanywa kwenye viwanja vya watu masikini kwa dhuruma” amesema Lukuvi.

Lukuvi amesema atapambana na viongozi hao pale ambapo atakuta majengo yamekithiri katika miji yao na hayana vibali vya ujenzi na baya zaidi majengo hayo yamejengwa katika maeneo ambayo hayaruhusiwi kujenga au yamejengwa katika kiwanja cha mtu mwingine na viongozi hao wameshindwa kufuatilia kwa kuyavunja au kuyaweka alama ya x majengo hayo, kwa kuwa huu ni uzembe unaotokea nchi nzima.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Kamishna Mstaafu Zelote Stephen amemhakikishia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi kuwa atayafanyia kazi mapendekezo yake kikamilifu na kwa haraka ili kuondoa migogoro na kero zinazoukabili mkoa wake katika masuala yote ya ardhi.
 

0 comments:

Post a Comment