Ni kipindi ambacho kaya zingekuwa zimevuna mazao mengi shambani na
zingepata ziada ya chakula ambayo ingeuzwa na kuwa na kipato cha kukidhi
mahitaji mengine muhimu. Hivi ndivyo ilivyokuwa imezoeleka katika
kipindi cha mavuno kati ya Mei na Julai.
Lakini sasa hali ni tofauti. Njaa na ukata umeshika kasi. Ukame na
mvua zisizotabirika zimesababisha upungufu wa uzalishaji mazao shambani.
Hali hii imezikumba kaya katika vijiji vya Buigiri, Chinangali II,
Mwegamile na Chamwino katika Tarafa ya Chilonwa, wilayani Chamwino,
Dodoma. Hivi ni sehemu ya vijiji 107 vilivyoko katika wilaya ya
Chamwino.
Wilaya hii ipo kilometa 40 kutoka katikati ya mji wa Dodoma ambao ni
makao makuu ya nchi. Wakazi wa vijiji hivi vilivyo jirani na ikulu,
wanalia njaa na kuwa tegemezi kwa chakula cha msaada. Mabadiliko ya
tabianchi ambayo ni mtiririko wa mfumo wa hali ya hewa, yamechangia
ukame na mvua zisizotabirika na kugeuka kichocheo cha umasikini kwa
wakazi hawa.
“Tumeambulia mabua matupu,” anasema Emily Oriyo, mkazi wa Chinangali
akielezea jinsi ambavyo uzalishaji umekuwa ukishuka mwaka hadi mwaka
kutokana na ukame. Wakati msimu mmoja wa mvua ambazo huanza Novemba na
kuishia Aprili, ulikuwa ukitumiwa na wakulima kuzalisha chakula na
kutosheleza mahitaji, hivi sasa mvua hazina kanuni.
Katika msimu huo mmoja, wakulima waliutumia kupanda mazao mbalimbali
na kuvuna, lakini Oriyo anaeleza namna ambavyo katika misimu mitatu
iliyopita, mvua imekuwa ikinyesha bila utaratibu huku kipindi cha ukame
kikiwa kirefu zaidi.
Oriyo anasema msimu wa mwaka 2016/17 umekuwa mbaya zaidi ya misimu
iliyopita. Mkulima huyu ambaye sasa anafanya vibarua, hususani kuponda
kokoto na kupata ujira wa Sh 1,000 kwa debe kutokana na kukosa chakula
na fedha, anasema mvua ya kwanza iliponyesha, Desemba 2016, alipanda
uwele katika ekari moja akitarajia kuvuna magunia 15. Lakini mkulima
huyu ameambulia debe tatu za uwele na alizeti, amepata debe moja na nusu
kutoka kwenye ekari moja.
Mkewe, Jane anakata kuni na kuuza mzigo kwa Sh 1,000. Familia hii ni
sehemu ya wakulima na wafugaji wa viji hivyo vya Chamwino, Chinangali
II, Buigiri na Mwegamile wanaolia na ukame na mvua zisizotabirika
zilizochangia kutozalisha na kusababisha njaa na ukata; hivyo kuongeza
umasikini. Mkazi wa Kijiji cha Buigiri, Olivia Chinyemba mwenye umri wa
miaka 59 anaeleza jinsi ambavyo katika miaka ya 1990 alivuna kuanzia
magunia matano ya mahindi na manane ya mtama kutoka kwenye ekari moja.
Lakini mwaka juzi (2015) alivuna magunia matatu ya mtama; Mwaka jana
alipata magunia mawili na mwaka huu amepata gunia moja la mtama katika
shamba lenye ekari moja huku mahindi akiwa amepata debe moja. Kwa upande
wake, Peter Mkasanga wa kijiji cha Buigiri, ambaye ni mfugaji,
anapolinganisha mwaka 1987 hadi 1990 na kipindi baada ya hapo, anasema
tatizo si kwenye chakula tu, bali pia malisho ya mifugo.
Baadhi ya wafugaji, wameuza mifugo kutokana na uhaba wa malisho.
Wakati huo huo ukosefu wa chakula na fedha, umewasukuma pia kuuza
ng’ombe. Kwa mfano, Mika Tozili wa kijiji cha Chamwino alikuwa na
ng’ombe 10 lakini mwaka huu amebakiwa na wanne. Wakilinganisha gharama
za kilimo na mavuno, wakulima wanaotumia wanyama kazi wanasema
wamejikuta katika hasara. “Ekari moja tunalima kwa Sh 30,000, palizi
gharama yake ni Sh 15,000 hadi Sh 20,000.
Sasa ekari moja unavuna debe moja la mtama na mahindi debe moja.
Unategemea umasikini utapungua?” anahoji Japhet Mdachi, mkazi wa
Buigiri. Debe la mahindi ambalo miaka miwili iliyopita liliuzwa kati ya
Sh 3,000 na 5,000 wakati wa kipindi cha mavuno, sasa linauzwa kati ya Sh
10,000 na Sh 13,000. Hii ni bei iliyowekwa kwa chakula cha msaada
kilichopelekwa katika vijiji hivyo.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwegamile, Jeremiah Mpanduka anaelezea kuwa,
Mei 2017, kaya zote 404 kijijini hapo, ziliidhinishwa kupata debe la
mahindi hayo ya msaada lakini baadhi ya familia, zilishindwa kumudu
kununua debe. “Si kaya zote zilimudu kununua mahindi hayo. Ilibidi
serikali ya kijiji iruhusu wanaoweza kununua kidogokidogo. Ndipo watu
wakawa wananunua kilo moja moja kadri wanavyopata fedha,” anasema.
Kila kaya ilipewa kibali cha kununua debe moja kwa Sh 15,000. Bei
hiyo ilikwenda hadi Juni walipojitokeza wafanyabiashara wengi walioanza
kupeleka mahindi kijijini hapo ndipo Agosti bei ilishuka hadi Sh 10,000.
Kulingana na maelezo ya wanakijiji kutoka kaya zinazotegemea kilimo,
wamekuwa wakipata mlo mmoja. Thomas Madimilo, mkazi wa Buigiri anaeleza:
“Kila nyumba ina njaa...
Ukipata chakula sasa hivi (saa 6 mchana), utegemee tena kula kesho
yake.” Kulingana na tathimini ya halmashauri, wilaya imetekeleza malengo
ya kilimo ya mwaka 2016/17 kwa asilimia 65 kutokana na mvua kunyesha
katika mtawanyiko usioridhisha hasa kipindi cha Januari hadi Machi,
2017. Jumla ya hekta 83,208 za mazao ya chakula zililimwa na kuzalisha
tani 82,569 za chakula wakati mahitaji halisi ya wilaya kwa mwaka ni
tani 87,518.
Hivyo wilaya inakabiliwa na upungufu wa uzalishaji wa tani 4,949 za
mazao ya chakula katika msimu wa 2017/18. Wakielezea hali ya uzalishaji
katika kilimo, wakulima 35 kati ya 40 niliozungumza nao, wanasema
hawajawahi kutembelewa na maofisa kilimo zaidi ya kupokea ushauri
kupitia mikutano ya hadhara ya kijiji. Hata hivyo, Newston Goi wa kijiji
cha Buigiri anawatetea maofisa kilimo akisema, kuwa ukame na mvua
zisizotabirika ziko nje ya uwezo wao.
Anatoa mfano kuwa yeye katika msimu wa 2016/17, alilima kwa kutumia
wanyama kazi, akapanda mbegu za muda mfupi na mbolea ya samadi. Lakini
bado hakuvuna kutokana na jua kali lililokausha mazao. “Hata maofisa
kilimo wakitutembelea na kutushauri, kama hakuna maji, hatuwezi kupata
mazao…
Sisi hatuwezi kutabiri kuwa mwezi huu tupande au tusipande,” anasema
Goi. Ofisa Mifugo wa Kata ya Buigiri, Stephano Adeline anakiri kuwa si
rahisi kumfikia kila mkulima na kumpa maelekezo ya kitaalamu. Kwa mujibu
wa ofisa mifugo huyu, Kata ya Buigiri ina kaya 4,032 ambazo kati yao,
wakulima ni 3,084 na wafugaji ni 948.
Anasema wamekuwa wakitumia mikutano ya hadhara kuwaelekeza wakulima
mbinu mbalimbali ikiwamo, kupanda mbegu za muda mfupi, kutumia mbolea na
kulima mtama na uwele badala ya mahindi. Kuhusu vitendea kazi hususani
vyombo vya usafiri kwa maofisa ugani, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri
ya Chamwino, Athumani Masasi anasema mwaka wa fedha uliopita, wilaya
ilinunua pikipiki 28 kwa ajili ya maofisa ugani wa kilimo na mifugo wa
kata 28 kati ya kata 36 zilizopo.
“Hata hivyo kutokana na kuongezeka kwa kata na vijiji wilaya
inaendelea kutenga bajeti ili kila afisa ugani wa kata awe na pikipiki,”
anasema mkurugenzi. Kwa mujibu wa sheria ndogo za kilimo za
halmashauri, majukumu ya maofisa ugani ni pamoja na kutoa programu ya
kilimo ya mwaka kulingana na hali ya hewa.
Programu itazingatia aina ya mazao kwa msimu, aina ya mbegu, namna na
wakati wa kupanda, namna na wakati gani wa kuvuna na kuhifadhi mazao
baada ya kuvunwa. Ataweza wakati wowote wa saa za kazi kuingia kwenye
eneo la kilimo kwa madhumuni ya kusimamia utekelezaji. Atatakiwa kuwa na
daftari linaloonesha idadi kamili ya wakazi na idadi ya ekari za mazao
ya kilimo.
Atapanga ratiba ya kutembelea mashamba ya wakazi ili kujionea kama
wanatekeleza wajibu wa kulima na kutunza mashamba. Hali kadhalika,
kulingana na mwongozo wa kitaifa wa Kilimo Kinachohimili Mabadiliko ya
Tabianchi uliozinduliwa Mei mwaka huu, maofisa kilimo wa vijiji na kata
wanaelekezwa kuhamasisha na kufundisha wakulima kutumia mbinu za kilimo
zinazohimili mabadiliko ya tabianchi.
Maofisa mipango na maofisa ugani wanaelekezwa kupanga na kuandaa
bajeti kwa ajili ya maendeleo ya kilimo kinachohimili mabadiliko ya
tabianchi katika jamii wanazozitumikia. Ofisa Mtendaji wa Kata ya
Buigiri, Boniphace Chikoti anasema katika ngazi ya kata, wamekuwa
wakiibua mambo wanayotaka yatekelezwe na halmashauri ikiwemo maombi ya
kuchimbiwa visima na malambo na kuyapeleka kwenye halmashauri ya wilaya.
Hata hivyo, Ofisa Mipango, Paschal Masatu anasema wao pia huangalia
vipaumbele kwa kuzingatia bajeti iliyopo. Lakini Ofisa Kilimo wa Wilaya,
Godfrey Mnyamale anafafanua kwamba, uwepo wa mipango si tatizo bali
tatizo ni utekelezaji ambao hutegemea upatikanaji fedha.
Anatoa mfano wa mwaka 2015/16-2016/17 kuwa fedha za maendeleo
hazikupatikana kama walivyohitaji jambo ambalo liliathiri utekelezaji wa
mipango iliyopitishwa na halmashauri katika vikao halali.
Mnyamale hakueleza kiasi cha fedha walichopokea na shughuli ambazo
ziliathirika kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha. Mkurugenzi wa
Halmashauri, Masasi anasema halmashauri ingetamani miradi ya umwagiliaji
iwe hata katika kila kijiji lakini ukosefu wa fedha za kuendeleza
miundombinu ya umwagiliaji hasa mabwawa, visima na nishati ya kusukuma
maji ndiyo sababu kubwa ya kutosambaza au /kujenga skimu kila kijiji.
Kwa mfano, skimu ya Buigiri ina eneo linalofaa kwa umwagiliaji lenye
hekta 9,191, lakini zinazotumika kwa umwagiliaji ni hekta 1,656.
Akielezea hatua zinazofanyika kuhakikisha fedha zinapatikana na
kunakuwapo na skimu za umwagiliaji vijijini, mkurugenzi anasema wilaya
inashirikisha sekta binafsi na serikali (PPP) katika ujenzi wa skimu
kama ya Chinangali II ambayo imekamilika kwa ushirikiano wa serikali,
wakulima na benki ya CRDB Wilaya imeshirikisha mashirika ya kimataifa
kwa kuandika andiko lililowezesha kupatikana fedha za ujenzi wa skimu za
umwagiliaji katika vijiji vya Fufu (ekari 100), Suli (ekari 100),
Chiboli (ekari 100) na Mvumi Makulu (ekari 140).
Mtaalamu wa mabadiliko ya tabia nchi na mazingira, Sixbert Mwanga
kutoka shirika la Climate Action Network (CAN - Tanzania) anafafanua
namna ambavyo inaweza kuwa vigumu kwa mkulima kuhimili mvua
zisizotabirika bila mbinu za upatikanaji maji.
Mwanga ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa CAN-Tanzania anasema, hata
wakulima wakipanda mbegu za muda mfupi kama vile mtama na uwele, endapo
zitakosa maji katika kipindi sahihi, hawawezi kupata mavuno.
Mwanga ambaye anasisitiza wakulima kupewa mbinu mbalimbali ikiwamo za
uhifadhi wa maji na udongo, anasema kuna hali ijulikanayo ‘dry spell’
(kipindi kirefu cha ukame) inaweza kufanya mkulima asivune.
Anasema mvua ya kwanza ikinyesha na mkulima akaanza kupanda,
inatakiwa ndani ya siku 30 tangu mbegu ipandewe, isitokee ukame kwa siku
10 mfululizo. “Ikitokea, basi ujue kuwa mkulima hawezi kuvuna,” anasema
Mwanga huku akisisitiza wataalamu wa kilimo kuwa karibu na wakulima kwa
lengo la kuwaelekeza mbinu mbalimbali za kuhifadhi maji ardhini.
Wakulima wa Chamwino ni sehemu ya asilimia 78 ya Watanzania
walioajiriwa katika sekta ya kilimo inayochangia zaidi ya asilimia 95 ya
mahitaji nchini. Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 inasema ifikapo mwaka
2025, maisha ya wananchi yawe bora na kuwepo utoshelevu na usalama wa
chakula.
Wednesday, October 25, 2017
Home »
» Athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyoongeza umasikini Chamwino
Athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyoongeza umasikini Chamwino
2:56 AM
1 comment
The Wizard of Oz - Casino Hotel, Bowling, Table Games
ReplyDeleteThe Wizard of 인천광역 출장안마 Oz is a new and 정읍 출장샵 adventurous The 춘천 출장샵 Wizard 울산광역 출장안마 is a new and adventurous casino hotel, bowling, table games, blackjack, craps, and bingo. Rating: 평택 출장안마 4.2 · 20 reviews