Thursday, August 20, 2015

FFU WATAWANYA MAANDAMANO YA MGOMBEA UBUNGE DODOMA

KIKOSI cha Kutuliza Ghasia (FFU) juzi kiliwatawanya Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumtia mbaroni mtu mmoja wakati wa msafara wa mgombea ubunge Jimbo la Dodoma Mjini, Antony Mavunde ukielekea Ofisi za CCM Wilaya.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya wanachama na wafuasi wa chama hicho kukaribia ofisi za Wilaya na kuonekana kuwa yalikuwa maandamano ambayo yamezuiwa kufanyika wakati wa wagombea kurudisha fomu. Yalijitokeza malumbano kati ya askari wa FFU na wafuasi wa CCM ambao walisisitiza kwamba walikuwa wakienda ofisi za chama.

Hata hivyo FFU waliwataka watawanyike kabla ya kumpiga mmoja wa wanachama, Mussa Idoha na kisha kumpakia kwenye gari la Polisi na kuondoka naye.

Askari hao ambao walikuwa kwenye magari mawili ilibidi waondoke na kada huyo na ndipo wananchi walipoamua kuandamana kwenda kituo kikuu cha Polisi kabla ya kutulizwa na viongozi wao.

“Mgombea ubunge wa Chadema alipokuwa akienda kuchukua fomu kulikuwa na maandamano makubwa ya magari na pikipiki lakini sisi wameamua kutukimbiza na kumpiga mmoja wetu,” alisikika mmoja wa wafuasi wa chama hicho.

Akizungumza na wananchi hao, Mavunde alisema kilichotokea ni faida kwao kwani wameiona nguvu ya CCM.

Aliwataka wananchi kutokubali kuwa wanyonge au sehemu ya kuchochea vurugu kwani walifuata taratibu zote za kisheria.

“CCM tunatakiwa kuwa kielelezo cha amani, wafuasi wa CCM walizuiwa na polisi lakini hakuna aliyetoa maneno ya kejeli na CCM itaendelea kuilinda amani,” alisema na kuongeza:
 
 “Sheria haikuvunjwa, maelezo ya Polisi yanasema walizuia watu kutembea kwa miguu walikuwa wakitaka msafara wa magari tu lakini tulipokuwa tunapita njiani, watu walianza kujitokeza wenyewe na ikawa ni vigumu kuwazuia.”

Awali, akizungumza baada ya kuchukua fomu, Mavunde aliwataka wananchi wa Dodoma kumchagua ili washirikiane kutatua changamoto zinazoikabili jamii.

0 comments:

Post a Comment