Friday, August 21, 2015

KIPINDUPINDU DAR CHAOGOPESHA WATU HATA KUPEANA MIKONO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadik amewataka wakazi wa jijini hilo kuchukua hadhari za kiafya ikiwamo kuacha kusalimiana kwa kushikana mikono kutokana na mlipuko wa kipindupindu ambao mpaka sasa umeshawapata watu 56, kati yao watatu wamefariki dunia.

Akizungumza jana ofisini kwake, mbali na kushikana mikono, Sadik aliwataka wananchi kuacha kunywa maji ya viroba maarufu kama “maji ya Kandoro” na juisi za mitaani ili kupunguza uwezekano wa kupata ugonjwa huo.

“Masuala ya kusalimiana mikono kwa mikono katika kipindi hiki tuepukane nayo lazima tunyanyapaliane wakati huu, ndiyo maana nilipoingia hapa sikuwapeni mikono kwa sababu nazingatia masharti ya madaktari,” aliwaambia waandishi wa habari.

Alisema ugonjwa huo ulilipuka Agosti 15 baada ya mtu mmoja kufariki dunia katika Hospitali ya Mwananyamala. “Hata familia yake, mke na watoto walipochukuliwa vipimo na wao walidhihirika kwamba wana maambukizi ya kipindupindu na mpaka sasa hivi bado tunao katika kituo chetu cha afya pale Mburahati,” alisema Sadik.

Alisema idadi ya wagonjwa imeongezeka hadi kufikia 56 lakini mpaka sasa wamebaki wagonjwa 36 katika kituo maalumu kilichofunguliwa Mbagala baada ya wengine kutibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Aliwataka wananchi kuepuka kula chakula kilichopoa na matunda ambayo hayajaoshwa. Alizitaja dalili za za ugonjwa huo kuwa ni kuharisha mfululizo, choo kuwa cha majimaji meupe kama ya mchele, kutapika mfululizo, ngozi kusinyaa, kiu kali, mdomo kukauka, mapigo ya moyo kuongezeka na mwili kukosa nguvu.

0 comments:

Post a Comment