Tuesday, August 25, 2015

Hisa za China zaanguka, masoko yatikisika ulimwenguni

Kuyumba kwa masoko ya hisa ulimwenguni, ambako kumesababisha hasara kubwa katika baadhi ya masoko tangu mwaka wa 2008 kutokana na kuanguka uchumi wa China, kumeongeza upya hofu kuhusu uthabiti wa uchumi wa ulimwengu.
Huku wachambuzi wa masuala ya fedha wakisema kuwa hofu ya kutokea tena migogoro ya kiuchumi ya mwaka wa 1997 na 2008 kwa kiasi kikubwa hayana msingi – hasa kwa sababu ya mageuzi yaliyofanywa tangu wakati huo – wameonya kuwa msukosuko unaoendelea kutokea China huenda ukauathiri ukuaji uchumi wa ulimwengu, hasa katika mataifa yanayoinukia kiuchumi.
Kuanguka kwa asilimia nane nukta tano ya soko la hisa la Shanghai hapo jana kulichochea kulivuruga kabisa masoko ya hisa nchini Marekani na Ulaya, huku kukiwa na viwango vilivyoshuka kabisa ambavyo viliondoa kabisa faida zozote zilizopatikana mwaka huu.
Hali ilikuwa ngumu hata zaidi katika mataifa yanayoinukia kiuchumi, na wakati masoko ya hisa yasiyo ya China yakionekana kurejea katika hali ya kawaida leo, bila shaka ulinganisho umefanywa na mgogoro wa kifedha wa mwaka wa 1997, ambao uliziacha nchi za Mashariki na Kusini mashariki mwa Asia katika hali mbaya na baadhi zikiomba misaada ya mikopo kutoka kwa Shirika la Fedha la Kimataifa – IMF

Katika wakati huo, China ilikuwa mwamba wa uthabiti. Mara hii, ndiyo chanzo cha msukosuko. Juhudi zilizoshindwa za Beijing kutuliza masoko yake yenyewe ya mtaji na kuzuia kudorora uchumi wake vilikwenda sambamba na kushuka ambako hakukutarajiwa kwa thamani ya sarafu ya yuan wiki mbili zilizopita.
Wasiwasi kuwa kushuka kwa thamani kwa sarafu ya yuan ni ishara kuwa uchumi wa nchi hiyo uko katika hali mbaya hata zaidi kuliko ilivyohifiwa – ijapokuwa China ni mojawapo ya nchi zinazokuwa kwa kasi kiuchumi duniani, utanuzi wa pato jumla la nchi umepungua kwa karibu asilimia saba – kulizusha hatua ya kuuza hisa zake.
Mataifa mengi yanayoinukia kiuchumi yakafuata mkondo huo, na kuchochea pambalo la ushindani wa kushuka kwa thamani ya sarafu.
Mchumi Angel Ubide kutoka Taasisi ya Uchumi wa Kimataifa ya Peterson anasema hofu kuwa viongozi wa Beijing hawajapata udhibiti wa matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo inaongezeka.
Charles Collyns, mchumi mkuu katika Taasisi ya Kimataifa ya Fedha mjini Washington anadokeza kuwa kuna sababu za kudumu ambazo zinaashiria kuwapo athari ya kudumu zaidi kwenye uchumi wa ulimwengu. Anasema kuna wasiwasi mpana kwenye masoko ya mataifa yanayoinukia kichumi, huku akiitaja migogoro ya kisiasa nchini Brazil na Uturuki, mageuzi yaliyokwama nchini India, athari za vikwazo dhidi ya Urusi na hasara ya mapato katika mataifa yanayouza nje mafuta kama vile Nigeria kutokana na kushuka bei za mafuta ambayo hayajasafishwa.
Kwa upande wa Japan, Ulaya na Marekani, vyanzo vya mgogoro wa mwaka wa 2008 ambayo ni mabenki yamefanyiwa mageuzi makubwa kupewa mitaji mipya ambayo inaziweka katika hali imara ya kukabiliana na misukosuko ya kifedha.
Tangu mwaka wa 2008, matrilioni ya dola katika sarafu zao rasmi yamewekezwa katika mataifa yao ili kuyaimarisha mabenki na kuongeza kukuza matumizi, uwekezaji na kuweka nafasi za ajira.
source: DW

0 comments:

Post a Comment