Tuesday, September 15, 2015

AJALI YA BASI LA METRO

Askari wa usalama barabarani na baadhi ya wananchi wakitazama basi la kampuni ya Metro, lililopinduka kwenye Barabara Kuu ya Segera-Chalinze, eneo la Mkata wilayani Handeni mkoani Tanga jana na kusababisha vifo vya abiria watano na wengine 39 kujeruhiwa. (Na Mpigapicha Wetu).

WATU watano wamekufa papo hapo na wengine 39 kujeruhiwa vibaya baada ya basi la Kampuni ya Metro, kuacha njia, kutumbukia bondeni na kupinduka.
Basi hilo lilikuwa likitoka Dar es Salaam kwenda Rombo mkoani Kilimanjaro.
Miongoni mwa waliokufa ni watatu wa familia moja, ambao ni baba, mama na binti yao mwenye umri wa miaka 12, wote wakazi wa mjini Moshi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
Alisema ilitokea majira ya saa 5 asubuhi kwa kuhusisha basi la kampuni ya Metro, aina ya Scania lenye namba za usajili T 442 DFA.
Alitaja waliokufa kwenye ajali hiyo ni Elimringi Minja (50), Eziwa Minja (47) na Haika Elimringi (12) ambao ni wa familia moja, Innocent Shayo (49) mkazi wa Moshi na Zakaria Kitumpa (43) mkazi wa mjini Korogwe mkoani Tanga.
Alisema basi hilo lililokuwa likiendeshwa na Raymond Urio, mkazi wa Kibamba, Dar es Salaam, lilipata ajali hiyo katika kitongoji cha Zimbabwe Kata ya Manga wilayani Handeni katika barabara kuu ya Segera - Chalinze.
“Baada ya basi kufika eneo hilo lenye kona, ghafla gari lilihamia upande wa kushoto wa barabara na kutoka, ndipo dereva akajaribu kulirejesha lakini bila mafanikio,” alisema.
Kamanda Mwombeji alisema; “Ndipo likamshinda kwa kuwa lilimvuta upande wa kushoto wakati akijaribu kukata hiyo kona na ndipo likaangukia kwenye bonde na kupinduka.”
Akizungumzia majeruhi 39, Kamanda huyo alisema 30 kati yao, walitibiwa katika Kituo cha Afya cha Mkata na kuruhusiwa kurejea nyumbani. Alisema wengine 9 hali zao sio nzuri.
“Majeruhi tisa bado wanatibiwa kwa sababu wameumia sehemu mbalimbali za mwili na huenda baadaye wakalazimika kuhamishiwa katika hospitali za wilaya za Handeni au Korogwe kwa matibabu zaidi kadri daktari atakavyoona inafaa,” alisema.
Alisema dereva wa basi hilo, alitoroka muda mfupi baada ya tukio na kwamba askari wanaendelea kumtafuta. Alisema uchunguzi kuhusu chanzo cha ajali hiyo, unaendelea.

0 comments:

Post a Comment