VINARA wa Ligi Kuu Tanzania Bara na mabingwa watetezi, Yanga, leo watakuwa tena kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania pointi tatu dhidi ya Tanzania Prisons ya Mbeya katika mechi ya raundi ya pili ya ligi hiyo.
Yanga ilianza ligi kwa kishindo Jumapili baada ya kuishinda Coastal Union ya Tanga kwa mabao 2-0 na hivyo kukalia usukani wa ligi hiyo, wakati Prisons ilipoteza mechi yake ya kwanza dhidi ya Azam FC kwa kufungwa mabao 2-1 hivyo leo inatafuta ushindi wa kwanza kwenye ligi hiyo.
Kocha wa Prisons, Salum Mayanga aliliambia gazeti hili jana kuwa ana imani timu yake itapata matokeo mazuri licha ya kukiri kuwa mechi hiyo haitakuwa nyepesi.
“Mechi itakuwa ngumu kama unavyojua Yanga ndio mabingwa watetezi hawatakubali kupoteza mchezo kirahisi, lakini nimeiandaa timu yangu baada ya kufanyia kazi makosa yaliyotokea kwenye mechi ya kwanza,” alisema kocha huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar.
Hata hivyo, mara nyingi Prisons imekuwa ikipata tabu kupata matokeo mazuri dhidi ya Yanga katika miaka ya karibuni. Yanga ndio inaongoza msimamo baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union katika mechi ya kwanza, hivyo leo inawania kuendeleza ushindi ili iendelee kukaa kileleni.
Akizungumzia mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Hans van Pluijm alisema hana wasiwasi na wachezaji wake.
“Kwanza nashukuru nimeshinda mechi ya kwanza, lengo langu kuendeleza ushindi katika mechi zote zinazofuata… sikatai ushindani lazima uwepo sababu kila timu imejiandaa kushinda,” alisema kocha huyo Mholanzi.
Mbali na mechi hiyo ya Dar es Salaam, kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, Simba inaendelea kuwa ugenini dhidi ya Mgambo Shooting. Simba ilishinda bao 1-0 katika mechi ya ufunguzi uwanjani hapo dhidi ya African Sports matokeo ambayo kocha wake, Dylan Kerr ametamba kuyaendeleza.
Kerr aliiongoza Simba kwa mara ya kwanza kwenye ligi mwishoni mwa wiki iliyopita na kutamba kuwa timu yake inao uwezo wa kushinda katika kila mechi. Kerr amekuwa akisema anataka kushinda mechi zote mbili za ugenini Tanga ili kuwapa wachezaji wake kujiamini.
“Ukishinda mechi ya kwanza ya pili na ya tatu timu inazoea kushinda na wachezaji wanajenga kujiamini katika mechi zinazofuata mpaka kutwaa ubingwa kila siku naamini hivyo,” alisema kocha huyo Muingereza. Mgambo ilianza ligi kwa sare dhidi ya Ndanda FC mjini Mtwara.
Majimaji baada ya kuifunga JKT Ruvu bao 1-0 katika mechi ya ufunguzi, leo itakuwa mwenyeji wa Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Mechi hiyo haitarajiwi kuwa nyepesi kwani kama Majimaji inatambia uwanja wake wa nyumbani, wapinzani wao Kagera Sugar walishinda bao 1-0 ugenini Sokoine dhidi ya Mbeya City hivyo si ajabu hata leo ikitamba ugenini.
Mbeya City na JKT Ruvu zitacheza Sokoine leo huku kila moja ikiwania ushindi wa kwanza baada ya kupoteza mechi za ufunguzi.
Kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga, Stand United itamenyana dhidi ya washindi wa pili wa msimu uliopita, Azam FC huku Toto African ikimenyana na Mtibwa Sugar uwanja wa CCM Kirumba Mwanza na Ndanda ikiikaribisha Coastal Union kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona.
Katika hatua nyingine, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limebaini kuwepo kwa vitendo vya wanafamilia wa soka Tanzania kujihusisha na masuala ya siasa wakiwa katika mavazi rasmi ya mpira yenye nembo za klabu na wadhamini wa Ligi.
Ikinukuu Katiba ya TFF Ibara ya I (4), taarifa ya shirikisho hilo jana ilieleza: “TFF inachukua fursa kuwakumbusha wana familia wote wa mpira wakiwemo viongozi, wachezaji, waamuzi, makocha na madaktari wa michezo kuwa ni marufuku kuelezea hisia zao za kisiasa au kujihusisha katika kampeni za kisiasa wakiwa katika mavazi rasmi ya mpira zikiwemo jezi na sare za michezo zenye nembo za TFF, vilabu wadhamini na ligi, Taifa Stars au za washirika wa TFF wakiwemo wadhamini.
“Aidha ni marufuku kwa mashabiki wa mpira kutumia fursa ya mechi za mpira wa miguu kubeba mabango au kusambaza ujumbe wa kisiasa. “Hatua kali zitachukuliwa kwa wataokiuka mahitaji ya katiba na kanuni za mashindano. TFF inatambua haki za wanamichezo kushiriki katika siasa ili mradi ushiriki wao hazikiuki kanuni na mahitaji ya Katiba za TFF na FIFA.”
Wakati huo huo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limepokea maombi ya Klabu ya Young Africans (Yanga) ya kutaka kufanya uchaguzi wake mkuu.
SHUDATE BLOG
0 comments:
Post a Comment