Thursday, September 17, 2015

KIPINDUPINDU CHAHAMIA DODOMA

Image result for KONGWA

WAKAZI wawili wa wilaya ya Kongwa mkoani hapa, wamefariki dunia baada ya kuugua ugonjwa wa kipindupindu.
Hayo yalielezwa jana Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Ezekiel Mpuya kufuatia kauli iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Donan Mmbando kuwa mkoa wa Dodoma ni miongoni mwa mikoa iliyoathiriwa na kipindupindu.
Akifafanua, Dk Mpuya alisema hivi karibuni walipokea mgonjwa mmoja wa kipindupindu kutoka Kijiji cha Mkoka Kata ya Mkoka wilayani Kongwa.
Alisema katika familia aliyotoka mgonjwa huyo, kulikuwa na mtu aliyekuwa ametoka mkoa wa Morogoro kwenye eneo ambalo linasadikiwa kuwa na ugonjwa wa kipindupindu na alisafiri hadi eneo la Mkoka bila ya wao kufahamu. Mtu huyo alikuwa na mtoto na alianza kuharisha.
“Mtoto huyo alipopelekwa kwenye Kituo cha Afya Mkoka na kuchukuliwa vipimo alibainika kwamba ni ugonjwa wa kipindupindu,” alisema.
Pia, Dkk Mpuya alisema hadi juzi kulikuwa na wagonjwa saba kwenye kituo hicho, ambapo wawili walifariki dunia, wawili waliruhusiwa na watatu bado wapo kituoni.
Alisema katika kijiji hicho cha Mkoka, kuna mwanakijiji mmoja naye alisafiri kuja Manispaa ya Dodoma, ambapo alionekana kuwa na dalili za ugonjwa huo.
“Alipoona dalili hizo aliamua kwenda kwenye Kituo cha Afya cha Makole na kuchukuliwa vipimo... ingawa vipimo vimeonyesha kuwa hana dalili za kuhara, lakini sisi tuna mashaka na tunaendelea kumhudumia,” alisema.
Dk Mpuya alisema walipotembelea kijiji cha Mkoka waligundua kuwa wakazi wengi wa eneo hilo hawana vyoo. Awali, Dk Mmbando alisema mikoa mitano ndiyo iliyoathirika na kipindupindu hadi sasa na hiyo ni Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Iringa na Morogoro.
SHUDATE BLOG

0 comments:

Post a Comment