Friday, September 11, 2015

KOMBE LA FA LITATIMUA VUMBI RASMI HIVI KARIBUNI



SASA ni rasmi kuwa Kombe la Shirikisho zamani FA linarejea msimu huu baada ya Kampuni ya Azam Media Limited kusaini mkataba wa miaka minne na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kudhamini michuano hiyo kwa mkataba wenye thamani ya Sh bilioni 3.3.
Kombe hilo litajulikana kwa jina la Azam Sports Federation Cup (ASFC) na litaanza Novemba mwaka huu. Katika hafla iliyofanyika Jengo la Kisenga LAPF, Kijitonyama, Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Jamal Malinzi alisema kwamba amefurahia kufanikisha azma ya kurejesha mashindano hayo.
Malinzi alisema kwamba duniani kote maendeleo ya soka yanatokana na kuwepo na mashindano mbalimbali yakiwemo ya Kombe la Shirikisho la nchi ambayo yanashirikisha na klabu za chini hadi zile zinazoshiriki Ligi Kuu.
“Nitafurahi sana kuona klabu ya Daraja la Pili inashinda Kombe hilo, duniani kote Kombe hili lipo na klabu za chini zimekuwa zikiwapiga ‘visu’ wale wakubwa,” alisema Malinzi. Aliongeza kuwa bingwa wa mashindano hayo atajinyakulia kitita cha Sh milioni 50 wakati kila timu itakayokwenda kucheza ugenini itapata Sh milioni tatu za safari na mwenyejii atapewa Sh milioni moja ya maandalizi.
“Tumeona bingwa wa michuano hii apate shilingi milioni 50 kwa sababu atakuwa amecheza mechi saba na yule wa Vodacom anayecheza michezo 30 anapata shilingi milioni 70,” aliongeza Malinzi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya TFF, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ alisema kuwa mashindano ya mwaka huu yatashirikisha klabu 64 na yataendeshwa kwa njia ya mtoano.
Kaburu ambaye pia ni Makamu wa Rais wa Simba, alizitaja timu hizo kuwa ni pamoja klabu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Bara, timu 24 za Daraja la Kwanza na idadi kama hiyo za Daraja la Pili. Alisema kwamba mshindi wa kombe hilo atapata nafasi ya kuiwakilisha nchi katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CAF) mwaka 2017.
Alieleza kuwa timu 16 za Ligi Kuu ya Bara zenyewe zitaanzia raundi ya pili itakayoshirikisha klabu 32 na kuongeza kwamba wiki ya mechi za Kombe la FA hakutakuwa na michezo ya Ligi ya Bara.
Hii ni mara ya kwanza kihistoria michuano ya Kombe la FA kuwa na udhamini na miaka ya imekuwa ikiibuka na ‘kuyeyuka’ tangu mwaka 1967 kabla ya kupotea moja kwa moja mwaka 2002.
Mara ya mwisho Kombe la FA lilifanyika mwaka 2002 na JKT Ruvu Stars ya Pwani iliibuka bingwa baada ya kuifunga Baker Rangers ya Magomeni kwenye fainali. Bingwa wa kwanza wa Kombe la FA enzi hizo likiitwa Kombe la FAT ilikuwa Yanga mwaka 1967, na michuano hiyo haikufanyika tena hadi mwaka 1985 Majimaji ya Songea ilipotwaa kombe.
Kombe la FAT likayeyuka tena kabla ya kurejea miaka 10 baadaye, 1995 na Simba SC ikatwaa ubingwa kabla ya kupokonywa na Sigara mwaka 1996, ambao nao walilitema kwa Tanzania Stars mwaka 1997 iliyofanikiwa kulitetea 1998 kabla ya kupokonywa na Yanga 1999.
Ubingwa wa FA mwaka 2000 ulikwenda kwa Simba waliopokonywa na Yanga SC mwaka 2001 kabla ya JKT Ruvu kuwa bingwa wa mwisho wa mashindano hayo mwaka 2002.
Ratiba ya mechi za ufunguzi raundi ya kwanza ni kati ya AFC vs Polisi Mara, Polisi Tabora vs Green Warriors, Kariakoo Lindi vs Changanyikeni Dar, Mkamba Rangers vs Ruvuma FC ya Kigoma, Rhino ya Tabora vs Alliance FC ya Mwanza, Panone vs Coca Cola Kwanza ya Mbeya na Polisi Moro vs Mshikamano Sports.
Nyingine ni Sabasaba Utd vs Abajalo ya Tabora, Magereza Iringa vs Polisi Dar, Mirambo vs Town Small Boys Ruvuma, Abajalo Dar vs Transcamp, Ruvu Shooting vs Cosmopolitan, Singida Utd vs Bulyhanhulu, JKT Rwamkoma vs Villa Squad, Wenda vs Madini Sports Arusha Pamba vs Polisi Dodoma.
SHUDATE BLOG

0 comments:

Post a Comment