Thursday, September 3, 2015

WATANZANIA SITA WALIOKUA WAMETEKWA WAACHILIWA HURU HUKO DRC




WATANZANIA sita waliokuwa wameshikiliwa mateka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wameachiwa huru usiku wa kuamkia juzi.
Hayo yalisemwa jana na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Liberata Mulamula, wakati akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam.
Balozi Mulamula alisema mateka hao walitekwa mwanzoni mwa mwezi uliopita Mashariki mwa Congo, Kivu Kaskazini ambako walikwenda huko kwa masuala ya dini ila kwa sasa wameachiwa huru.
“Hii ni mara ya kwanza kwa tukio kama hili kutokea kwa Watanzania kutekwa ila tunashukuru kwa sasa wapo huru na wanaelekea Goma kwa ajili ya kukutana na Balozi wa Tanzania nchini Congo ili taratibu nyingine zifuatwe,” alisema Balozi Mulamula.
Aliongeza kuwa inasemekana walitekwa na kundi la waasi ambalo mpaka sasa halijajulikana na walitoa masharti kuwa wanataka Dola za Marekani 20,000 (zaidi ya Sh milioni 60).
“Hakuna fedha yoyote iliyotolewa ili kuwakomboa japo wapo watu waliojitokeza kuchangia ikiwemo raia wa Congo na familia za mateka hao, lakini fedha hizo hazijatolewa kwa waasi hao na hatujui imekuaje mpaka wakawaachia huru,” aliongeza Katibu Mkuu.

Shudate Blog

0 comments:

Post a Comment