Friday, September 11, 2015

VPL KUANZA HII LEO MSIMU 2015-16

Image result for vodacom premier league 2015/16

MSIMU wa Ligi Kuu ya soka ya Tanzania Bara 2015-2016 unaanza leo kwa timu 14 kati ya 16 zikitarajiwa kushuka dimbani kuwania pointi tatu za kwanza.
Timu zitakazoshiriki ligi hiyo inayochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini, ni mabingwa watetezi, Yanga ya Dar es Salaam pamoja na mahasimu wao wa jadi, Simba, Azam FC zote za Dar es Salaam.
Nyingine ni timu tatu za Tanga, Coastal Union, Mgambo JKT na African Sports, Mtibwa Sugar (Morogoro), JKT Ruvu (Pwani), Stand United na Mwadui FC (Shinyanga), Toto Africans (Mwanza), Majimaji FC (Ruvuma), Kagera Sugar (Kagera), Ndanda FC (Mtwara), Mbeya City na Tanzania Prisons (Mbeya).
African Sports, Toto Africans, Mwadui na Majimaji FC ni timu zilizopanda daraja msimu huu, ingawa zote kwa nyakati tofauti zimewahi kucheza katika ligi hiyo kubwa zaidi katika soka Tanzania Bara.
Bingwa mtetezi Yanga hataishuka dimbani leo, badala yake itaanzia nyumbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho dhidi ya Wagosi wa Kaya, Coastal Union ya Tanga.
Azam FC ambayo ilipokonywa ubingwa na Yanga msimu uliopita, itaanzisha mbio za ubingwa huo msimu huu leo kwa kuikaribisha Tanzania Prisons ya Mbeya kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Simba baada ya kukosa ubingwa kwa misimu mitatu mfululizo, leo ataanzia ligi ugenini mkoani Tanga ambako atakuwa mgeni wa African Sports iliyorejea katika ligi ilikopotea kwa zaidi ya miaka 20.
Mechi nyingine leo zitaikutanisha Mbeya City dhidi ya Kagera Sugar (Sokoine, Mbeya), Ndanda FC dhidi ya Mgambo JKT (Nangwanda Sijaona, Mtwara), Majimaji itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu (Majimaji, Songea), Stand United itaialika Mtibwa Sugar (Kambarage, Shinyanga) na Toto Africans dhidi ya Mwadui FC (CCM Kirumba, Mwanza).
Yanga itakuwa ikiwania taji lake la 26 la ubingwa wa Tanzania Bara huku ikijivunia kikosi kilichosheheni wachezaji mahiri wa ndani na nje ya nchi chini ya makocha Hans van Pluijm na Charles Boniface Mkwasa.
Ikijivunia uongozi wa mfanyabiashara maarufu nchini, Yusuf Manji, Yanga imesajili wachezaji mahiri wa kigeni, Donald Ngoma, Thabani Kamusoko na Vincent Bossou ambao watacheza ligi ya Tanzania kwa mara ya kwanza, wakiungana na wageni wenzao waliopo Amissi Tambwe, Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite na Andrey Coutinho.
Pia inao wachezaji wengine mahiri wapya watakaovaa jezi za kijani na njano kwa mara ya kwanza katika ligi ambao ni Haji Ngwali, Deus Kaseke, Geoffrey Mwashiuya, Matheo Simon, Mudathir Hamis na Benedict Tinoco.
Wapya hao wa kigeni na wa nyumbani wataungana na wengine waliocheza msimu uliopita wakiongozwa na nahodha Nadir Haroub na mfungaji na mchezaji bora wa ligi msimu uliopita, Simon Msuva wanaotarajiwa kuifanya iendelee kutamba na kutajwa kuwa miongoni mwa timu mbili zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.
Nyingine ni Azam FC ambayo baada ya kukosa ubingwa ilimrejesha kocha wake wa zamani, Mwingereza Hall Stewart ambaye aliipa taji lake la kwanza la Kombe la Kagame mapema mwezi uliopita.
Hall anajivunia mchanganyiko wa wachezaji nyota wa kigeni na wa nyumbani ambao waliifanya ishike nafasi ya pili msimu uliopita na pia kuipa ubingwa wa Kagame wakiongozwa na nahodha John Bocco.
Mbali ya hao, imesajili nyota wa kigeni kama Jean Baptise Mugiraneza, Allan Wanga, na wa nyumbani kama Ramadhani Singano na Ame Ally ambao watavaa jezi za timu hiyo kwa mara ya kwanza katika Ligi Kuu.
Kwa upande wa Simba, ilimaliza ligi ikiwa katika nafasi ya tatu chini ya kocha Goran Kopunovic wa Serbia ambaye baadaye alitupiwa virago vyake na kuletwa Dylan Kerr, raia wa Uingereza mwenye kibarua cha kuhakikisha anapeleka ubingwa Msimbazi ambako umekosekana tangu msimu wa 2011/2012.
Simba imesajili wachezaji wa kigeni kama timu nyingine kwa kuleta Justice Majabvi, Pape N’daw, Vincent Angban, Emily Nimuboma, Hamis Kiiza aliyewahi kung’ara akiwa Yanga, ambao wanatarajiwa kuongeza nguvu katika kikosi kilichomaliza msimu.
Pia imesajili wachezaji wa nyumbani wapya kama Samir Nuhu, Peter Mwalyanzi, Mwinyi Kazimoto na Mussa Hassan ‘Mgosi’ waliorejea tena kikosini, Danny Lyanga na Joseph Kimwaga aliyetokea Azam kwa mkopo.
Timu hizo tatu zinatarajiwa kupata upinzani mkubwa kutoka kwa timu nyingine kama Mwadui, Mtibwa Sugar, Majimaji na Stand United ambazo si tu zimesajili vizuri, bali nyingine zina udhamini mnono.
Kocha Mkuu wa zamani wa Taifa, Taifa Stars, Dk Mshindo Msolla ambaye licha ya kuzipa nafasi ya kutamba baadhi ya timu, anazipa nafasi kubwa zaidi Yanga na Azam FC.
“Pamoja na yote hayo, bado nazipa nafasi mbili timu za Yanga na Azam. Nazipa nafasi kwa sababu moja, zimefanya usajili mzuri, zimecheza mechi nyingi za majaribio, tena za kimataifa, zimeshiriki Kombe la Kagame kwa hiyo makocha wao wamepata nafasi ya kuona kasoro na kuzirekebisha. “Wamekuwa na mechi nyingi za majaribio, tena za kimataifa, nina uhakika makocha wao wanafahamu nani aanze katika timu zao na nani mbadala wake katika benchi,” alisema Dk Msolla.
“Kwa Simba, wamefanya kosa kubwa la kiufundi, wamesajili timu halafu wamemtafuta kocha. Mwalimu ndiye anayesajili timu kwa kufuata mipango yake kwa kuangalia mapengo katika timu iliyomaliza ligi na mahitaji kwa maana aina ya mfumo anaotaka kuutumia. Wachezaji wamesajiliwa na viongozi, hili halinipi matumaini,” alieleza.
“Lakini timu nyingine ambayo msimu huu itafanya vizuri ni Mtibwa Sugar. Hii inatokana na ukweli kuwa haibadiliki sana na pia imewarudisha wachezaji wake wa zamani wenye uwezo. Yupo Javu (Hussein) na Bahanuzi (Said) na yule kipa wao (Hussein Sharrif), hawa wataisaidia kwa kuungana na wa zamani. “Lakini pia naipa nafasi Mwadui. Imesajili vizuri na imecheza mechi nyingi za majaribio, karibu mechi kumi, tena na timu zote kubwa kasoro Yanga. Hii itatoa upinzani mkubwa sana,” alieleza Dk Msolla katika mahojiano ambayo yameandikwa katika moja ya kurasa za gazeti hili leo.
Timu tatu za mwisho zitashuka daraja baada ya ligi kumalizika Mei 7, mwakani, ambayo ina udhamini mnono wa Kampuni ya simu ya Vodacom, Kampuni ya Azam Media Limited na pia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) katika masuala ya afya ya wachezaji na viongozi wa timu kuanzia msimu huu.
shudate blog

0 comments:

Post a Comment