kocha wa Mwadui Fc
TIMU ya Mwadui FC kati ya timu nne zilizopanda msimu huu inapewa nafasi ya kuleta upinzani mkali katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara kutokana na kusajili wachezaji wenye uzoefu.
Mwadui, Toto Africans, Majimaji na African Sports ndizo timu nne zilizopanda daraja msimu huu zikitarajiwa kuleta upinzani huku wachambuzi wakiiweka kileleni miongoni mwa timu hizo. Mbali na wachambuzi, pia wachezaji wazamani nao wameupa timu hiyo nafasi kubwa ya kufanya vizuri.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti mchezaji wa zamani wa Yanga na mchambuzi wa Soka, Ally Mayay na golikipa wa zamani wa Simba, Mosses Mkandawile walisema Mwadui ndio timu pekee itakayosumbua timu kongwe wakitoa sababu mbalimbali.
Mayay alisema Mwadui itafanya vizuri kwa kuwa ina wachezaji wenye uzoefu na ligi na pia kocha wake, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ ni mshindani ambaye anapambana kuona timu yake inafanya vizuri.
“Tumeona Mwadui imefanya usajili mzuri na imecheza mechi mbalimbali za kirafiki na kufanya vizuri, hii ndio timu itakayoleta upinzani ukilinganisha timu hizo nyingine zilizopanda daraja,” alisema.
Alisema nafasi ya pili anatoa kwa African Sports ya Tanga ambayo imeonekana kufanya vizuri kiasi katika mechi za kirafiki ingawa maandalizi yao hayakuwa mazuri sana na nafasi ya tatu akiipa Toto Africa ya Mwanza na ya mwisho Majimaji ya Songea.
Alisema Toto Africa ni timu nzuri na kongwe lakini kuna matatizo kwenye uongozi huku Majimaji akisema imefanya usajili lakini anahofia katika maandalizi yao kutokuwa mazuri sana.
Naye, Mkandawile pia anaipa Mwadui nafasi ya kwanza kwa kigezo alichotoa Mayai cha kuwa wachezaji wenye uzoefu na kuangalia tathmini ya mechi za kirafiki, nafasi ya pili akiipa Toto African kwa kuamini kuwa ina Kocha mgeni akisaidiwa na mzoefu ambaye ni Jerryson Tegete mwenye uzoefu na ligi.
Alisema nafasi ya tatu anaipa Majimaji kutokana na maandalizi yao na nafasi ya mwisho akiipa African Sports ambao pia wamejizatiti kufanya vyema. “Kulingana na maandalizi ya timu hizo kuanzia usajili na mechi za kirafiki walizocheza, timu kongwe zisitegemee kama zitapita kiurahisi, kutakuwa na upinzani mkali,” alisema.
SHUDATE BLOG
0 comments:
Post a Comment