Wednesday, September 9, 2015

NHIF KUWAPA BIMA WACHEZAJI WA MPIRA TANZANIA


Image result for TFF

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeingia makubaliano na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) wa kuzihudumia klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara. Katika makubaliano hayo, klabu za Ligi Kuu zitawajibika kuwalipia wachezaji wao kiasi cha Sh 76,800 kwa kila mchezaji kwa mwaka mzima, ambapo inalihusu pamoja na benchi la ufundi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana katika ofisi za TFF, Ofisa Habari Mwandamizi wa NHIF, Luhende Singu alisema kuwa makubaliano hayo yana tija zaidi kwa wachezaji na klabu zao kwa kuwa yamepunguza gharama.
Alisema kuwa kutokana na udhamini wao huo kwa sasa, klabu inatakiwa kulipia kiasi kisichozidi Sh milioni mbili unusu wakati kama iwapo ingegharamikia klabu yenyewe kuwalipia bima wachezaji wake ingelipa hadi Sh milioni tano kwa mwezi.
Alisema kuwa katika makubaliano hayo ya msimu mmoja, wachezaji wanaweza kutibiwa katika hospitali zote ambazo ni mwanachama wa NHIF kuanzia za Dar es Salaam hadi zile za mikoani.
Alisema kuwa mchezaji atatabiwa kila aina ya ugonjwa unaotibiwa chini ya bima hiyo kuanzia malaria na matatizo mengine. Aliongeza kuwa kwa kuanzia watatibiwa wao wachezaji na wahusika wa benchi la ufundi lakini kwa baadae watakuja kutibiwa na wategemezi wao.
"Huu mfumo umeamua kuhakikisha kuwa unawasaidia wachezaji hawa kupata huduma za afya kwa bei nafuu na kwa sasa ndio tumeingia makubalinao na wachezaji hawa kupitia klabu zao," alisema Singu.
Aliongeza: "Kama klabu zingetakiwa kujilipia basi ingekuwa ni fedha nyingi ila kwa sisi tumeamua kuwasaidia hawa wachezaji kwa staili hii na hiyo ni kuonesha kwetu kwa kiasi gani tunajali afya za wachezaji kwa mustakabali wa ukuaji wa michezonchini.”
Aliongeza kuwa klabu za Ligi Kuu zinatakiwa kufanikisha mapema uandikishwaji wa majina ya wachezaji wao haraka ili taratibu za kupatiwa bima hiyo uanze. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa alisema kuwa, NHIF imeubeba mzigo huo mkubwa ambao klabu za Ligi Kuu zilishindwa kuubeba.
Alisema kuwa kwa muda mrefu klabu hizo zilikuwa zikielemewa na utoaji wa huduma za bima ya afya kwa wafanyakazi wake na walipokuwa wakiumwa hali ilikuwa ni mbaya zaidi.

0 comments:

Post a Comment