KIKOSI cha Simba kinatarajia kuondoka leo kwenda Tanga kwa ajili ya mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara inayotarajiwa kuanza Jumamosi dhidi ya African Sports ya huko.
Simba ilipiga kambi Zanzibar kwa maandalizi ya ligi hiyo kwa takribani wiki mbili zilizopita. Msemaji wa Simba, Haji Manara alisema jana kikosi chake kipo tayari kuanza ligi.
“Timu imemaliza rasmi kambi yake Zanzibar na kesho (leo) itafanya safari ya kwenda Tanga, tunatarajia kupata matokeo mazuri kwenye mechi hiyo,” alisema.
Simba inasaka ubingwa kwa udi na uvumba baada ya kuukosa kwa zaidi ya misimu mitatu. Kocha Mkuu wa timu hiyo, Dylan Kerr alisema ana imani timu yake itaibuka na ushindi katika mechi hiyo ya kwanza na ile ya pili dhidi ya Mgambo Shooting itakayochezwa Septemba 16 huko huko Tanga.
Kerr ameifuatilia African Sports ikicheza mechi ya kirafiki na Coastal Union mwishoni mwa wiki iliyopita na kusema hashindwi kuifunga. Simba baada ya kucheza na African Sports, itashuka dimbani kwenye uwanja huo kucheza na Mgambo JKT Jumatano ijayo.
Kerr alisema lengo lake ni kushinda mechi hiyo ili kuwaondoa woga wachezaji wake katika mechi zijazo.
“Kwenye soka unapoanza vizuri mechi ya kwanza unajijenga kujiamini mechi zijazo, utashinda ya pili na ya tatu na kuendelea na mwisho kutwaa ubingwa, nataka kushinda mechi ya kwanza kuwafanya wachezaji wangu wajiamini,” alisema.
0 comments:
Post a Comment