Friday, September 4, 2015

TAIFA STARS YAIUMIZA KICHWA TIMU YA TAIFA YA NIGERIA

Kocha wa timu ya Taifa ya Nigeria, Sunday Oliseh.


KIWA imesalia siku moja kabla ya mechi ya timu ya soka ya taifa, Taifa Stars dhidi ya Nigeria, kocha Sunday Oliseh ameonesha hofu akisema hawafahamu wapinzani wake.
Aidha kocha huyo amekuwa na wasiwasi na kocha wa Yanga, Hans van Pluijm kwamba atampa kocha Charles Mkwasa mbinu za kuiua Nigeria. Taifa Stars kesho itaikaribisha Nigeria kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam katika mechi ya kuwania kufuzu michuano ya Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2017.
Akikaririwa kwenye mtandao wa Supersport jana, Oliseh alisema amekuwa akifuatilia mikanda mbalimbali ya video za michezo ya Stars, lakini amekuwa gizani kuifahamu vizuri timu hiyo.
Oliseh alikiri kwamba yeye na makachero wake hawajaiona mikanda ya mechi za Stars chini ya kocha mpya Mkwasa na hivyo wako gizani kwani hawafahamu Stars itaingia vipi uwanjani kesho.
Oliseh aliyasema hayo akiwa Abuja juzi: “Tanzania ni timu isiyotabirika na kwa maana hiyo tunaweza kupata mshangao katika mechi hiyo kwa sababu hatufahamu falsafa ya kocha mpya na wanacheza nyumbani,” alisema.
Kitu kimoja ambacho Oliseh ana uhakika nacho ni kwamba Mkwasa atakuwa amepewa mbinu nakocha Mkuu wa Yanga Hans van Der Pluijm. Mkwasa ni msaidizi wa Van Pluijm Yanga.
Pluijm aliyewahi kufanya kazi Ghana katika klabu za Kotoko na Chelsea Berkum anaifahamu soka ya Afrika Magharibi na hakuna ubishi kwamba atakuwa na mbinu kadhaa alizowekeza kwa Mkwasa.
Kambi ya Nigeria imeingia hitilafu kwani licha ya kuondoka kwa Joel Obi kutokana na kuwa majeruhi, nahodha wa timu hiyo Enyama amefiwa na mama yake. Stars ilikuwa Uturuki kwa kambi ya wiki moja na ilirejea nchini juzi tayari kwa mechi hiyo.
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mkwasa aliliambia gazeti hili kuwa wanaifahamu Nigeria ni timu kubwa lakini hawaiogopi na wako tayari kukutana nayo. “Tunashukuru tumefika sala nyumbani na tupo tayari kwa ajili ya mechi ya Jumamosi (kesho)…
Ninachoweza kusema ni kwamba wapinzani wetu tunawafahamu na wanafahamika kutokana na uwepo wao wa mara kwa mara kwenye michuano ya kimataifa, lakini mimi na timu yangu hatuliogopi hilo, tutakachokifanya ni kupambana nao mwanzo mpaka mwisho,” alisema.
Stars inaingia uwanjani kesho ikitoka kufungwa mabao 3-0 dhidi ya Misri huku wapinzani wake Nigeria wakitoka kushinda mabao 2-0 dhidi ya Chad katika mechi zilizochezwa Juni mwaka huu.
Kwa mujibu wa viwango vya ubora wa Fifa vilivyotolewa jana, Tanzania imeachwa na Nigeria kwa nafasi 87 ikishika nafasi ya 140 huku wapinzani wao wakiwa kwenye nafasi ya 53.

SHUDATE BLOG

0 comments:

Post a Comment