Tuesday, September 15, 2015

JK: Ndoto kuipaisha Kigoma zinatimia

Image result for kikwete

RAIS Jakaya Kikwete amesema ndoto yake ya kuuona mkoa wa Kigoma ukileta mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini imeanza kutimia, kutokana na kuanza kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya kiuchumi.
Aidha, amewahakikishia wananchi wa mkoa huo, kuwa mkoa huo sasa utaunganishwa na mikoa mingine ya Kanda ya Magharibi kwa barabara za lami.
Rais Kikwete aliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani hapa.
Awali, akizindua jengo la kitega uchumi la Shirika la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) alieleza kuwa katika kipindi kifupi kijacho, mkoa wa Kigoma utapiga hatua kubwa za kimaendeleo nchini.
Katika kuhakikisha mpango huo unafanikiwa, alisema kuwa serikali inakamilisha mpango wa kuleta meli mbili za abiria katika Ziwa Tanganyika sambamba na uboreshaji wa miundombinu ya reli na bandari.
Rais Kitwete amesema mkoa wa Kigoma ni moja ya mikoa ambayo miaka michache ijayo itapiga hatua kubwa kimaendeleo katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii.
Akizungumzia kufunguliwa kwa jengo hilo la kiuchumi la NSSF, Rais Kikwete alisema ni kichocheo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi mkoani humo na kwamba shirika hilo limetambua fursa za kiuchumi zilizopo mkoani Kigoma na kuweza kuzitumia.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk Ramadhani Dau, alimweleza Rais Kikwete kiasi cha Sh bilioni 7.6 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo la kitega uchumi na kwamba hadi kukamilika kwake ujenzi wake umetumia kampuni zote za Kitanzania.
Dk Dau alisema hadi sasa tayari asilimia 85 ya jengo hilo limeshapangishwa kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ambao wamefungua ofisi ambapo sambamba na mradi huo pia shirika hilo linatekeleza mradi wa ujenzi wa kituo cha kimataifa cha biashara katika eneo la Mwandiga nje kidogo ya manispaa ya Kigoma Ujiji ambao unatarajia kugharimu kiasi cha Sh bilioni 43.7.
Akizungumza katika uzinduzi wa jengo hilo, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, alisema kuwa NSSF imeendelea kutekeleza agizo la Rais la kuitaka mifuko ya jamii kuwekeza katika maeneo ya kusaidia jamii, likiwemo suala la mikopo kwa wakulima na wajasiriamali wadogo.
Kabla ya uzinduzi wa jengo la kitega uchumi la NSSF, Rais Kikwete alizindua jengo la kitega uchumi la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Barabara ya Lumumba mjini Kigoma sambamba na uzinduzi wa nyumba 36 za gharama nafuu zilizojengwa eneo la Mlole mjini hapa.
Akitoa maelezo kwa Rais, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Nehemia Mchechu, alisema ujenzi wa nyumba hizo ni utekelezaji wa agizo la Rais la kujenga nyumba za gharama nafuu kila mkoa na kwamba nyumba zote zilizokwishajengwa mkoani Kigoma zimepata wateja.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, alimweleza Rais Kikwete kuwa uzinduzi wa jengo hilo la kitega uchumi na nyumba hizo za makazi za gharama nafuu ni utekelezaji wa mpango wa kulipandisha hadhi shirika hilo ili kuingia kwenye ushindani wa kibiashara.
Lukuvi alisema pamoja na hilo serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ambayo yatawezesha shirika hilo kuendelea na mpango wa ujenzi wa nyumba bora za gharama nafuu katika wilaya zote nchini pamoja na ujenzi wa majengo ya vitega uchumi.
Barabara za lami Mapema jana, alizindua barabara ya Kidahwe - Uvinza iliyojengwa kwa kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita 76.6 iliyogharimu Sh bilioni 82.044.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, alisema: “Katika serikali yangu ya awamu ya nne nimefanya jitihada kubwa za kufungua barabara za ukanda wa Magharibi, mkoa huu wa Kigoma ulikuwa kama kisiwa na nikasema hali hii haikubaliki lazima tufungue barabara.”
Alisema kila upande mkoa wa Kigoma wamejitahidi kuufungua kwa kujenga barabara na kuunganisha na mikoa mingine ili kurahisisha usafiri na kukuza mawasiliano ya kiuchumi.
“Kama mkimchagua Dk John Magufuli ambaye anazijua barabara hizi atamalizia palipobaki, kwa kuwa kazi hiyo anaijua hivyo kumrahisishia utendaji wake… siyo kwamba nampigia kampeni ila penye ukweli lazima tuseme,” alisema.
Alishukuru serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu pamoja na Mfuko wa Abu Dhabi kwa kufadhili ujenzi wa barabara hiyo na kuwataka wananchi kuitunza ili iweze kuwanufaisha kiuchumi kwa muda mrefu.
“Barabara hii niliweka jiwe la msingi Julai 4 mwaka 2011 na nimefurahi kuizindua kabla sijang’atuka. Nina imani itafungua mkoa wa Kigoma kiuchumi hasa katika usafirishaji wa abiria, bidhaa na kuongeza maendeleo ya mkoa”.
Mapema Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara, Patrick Mfugale alisema barabara hiyo ni sehemu ya barabara ya Kigoma-Uvinza-Kaliua- Tabora ambayo inafupisha safari ya Tabora- Kigoma kwa zaidi ya kilomita 300 ikilinganishwa na njia ya Tabora- Nzega- Kigoma.
Alisema mradi huo umegharamiwa kwa pamoja na serikali ya Abu Dhabi kupitia mfuko wake wa maendeleo wa Abu Dhabi(ADFD) iliyochangia asimia 73 ya gharama na serikali ya Tanzania iliyochangia asilimia 27 ya gharama ikiwa ni pamoja na fidia kwa walioathiriwa na mradi.
Mfugale alisema kampuni iliyoshinda zabuni ya ujenzi wa mradi huo ni ya China Henan International Co-operation Group Co. Ltd (CHICO) ya China kwa gharama ya Sh bilioni 78.241 na kwa muda wa miezi 34 ikiwa ni pamoja na muda wa maandalizi wa miezi mitatu.
Kwa upande wake, Balozi wa Falme za Kiarabu nchini, Abdullah Ibrahim alisema ufunguzi wa barabara hiyo utasaidia kufungua masoko na biashara za kukuza uchumi na hiyo inatokana na juhudi za Rais Kikwete na kuahidi ushirikiano zaidi kwa ajili ya maendeleo ya nchi hizo.
Kukamilika kwa barabara ya Uvinza- Kidahwe- Urambo- Itigi- Manyoni kunafungua huduma za usafirishaji wa bidhaa, mizigo katika mkoa wa Kigoma na hivyo kuunganisha maeneo mengine ya nchi na kuhuisha fursa ya wananchi kiuchumi.
SHUDATE BLOG

0 comments:

Post a Comment