SERIKALI imetakiwa kufanya mabadiliko makubwa ya kisera kuwezesha kukua kwa viwanda vidogo na vya kati nchini.
Kauli hiyo imo katika utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) kuhusu ukuaji wa sekta hiyo katika muktadha wa upatikanaji wa fedha.
Akiwasilisha utafiti huo mmoja wa watafiti, Hossana Mpango alisema kwamba kwenye utafiti wao wamebaini mgongano mkubwa wa kisera na utendaji, unaosababisha kukwama kwa maendeleo ya sekta hiyo.
Alisema ingawa kuna tatizo kubwa la ajira ambalo limefanya watu wengi kukimbilia kujiajiri wenyewe, kuna changamoto kubwa katika sekta hiyo hasa sera na uwapo wa mlolongo wa taasisi zinazopishana mamlaka na huku wakiwa ndio wanatoa leseni wachukua tozo.
Alizitaja taasisi hizo zinazopishana mamlaka kama Shirika la Viwango nchini (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Mamlaka ya Mapato (TRA) halmashauri mbalimbali.
Alisema mabadiliko ya kisera yatawezesha kutengeneza muundo unaojali ukuaji wa sekta hiyo hasa kwa kuangalia kodi zinazolipwa ambazo kwa sasa ni za aina moja bila kuangalia uwekezaji unaohusika.
Alisema mabadiliko ya kisera yatasaidia kuimarisha sheria na kuweka sawa mwelekeo wa sekta hiyo kwa kuzingatia kwamba inahitaji mchango mkubwa wa nje wa kifedha ili kukua.
Pia utafiti huo ulishauri kwamba serikali ni lazima kutenga fungu ambalo litatumiwa na taasisi kama SIDO, NEEC na hata maofisa biashara wa wilaya kwa ajili ya mafunzo ya uajasiriamali na uendeshaji wa biashara.
Mapema Mkuu wa idara ya utafiti na machapisho wa ESRF, Profesa Fortunata Makene aliwataka washiriki wa warsha hiyo kutoa michango katika kuboresha uelewa ili serikali iweze kutatua kizungumkuti cha ukuaji wa sekta hiyo.
SHUDATE BLOG
0 comments:
Post a Comment